1 Wafalme 2:25-46
25
Hivyo Mfalme Solomoni akatoa amri kwa Benaya mwana wa Yehoyada, naye akampiga Adoniya akafa.
26
Mfalme akamwambia kuhani Abiathari, “Nenda huko Anathothi katika mashamba yako. Wewe unastahili kufa, lakini sitakuua sasa, kwa sababu ulilichukua Sanduku la Bwana Mwenyezi mbele ya Daudi baba yangu na ulishiriki taabu zote za baba yangu.”
27
Hivyo Solomoni akamwondoa Abiathari kwenye ukuhani wa Bwana, akilitimiza neno la Bwana alilokuwa amenena huko Shilo kuhusu nyumba ya Eli.
28
Habari zilipomfikia Yoabu, ambaye alikuwa amefanya shauri baya na Adoniya, lakini sio na Absalomu, alikimbilia kwenye hema la Bwana na kushika pembe za madhabahu.
29
Mfalme Solomoni akaambiwa kuwa Yoabu amekimbilia kwenye hema la Bwana naye alikuwa kando ya madhabahu. Basi Solomoni akamwagiza Benaya mwana wa Yehoyada: “Nenda ukamuue!”
30
Ndipo Benaya akaingia kwenye hema la Bwana na kumwambia Yoabu, “Mfalme anasema, ‘Toka nje!’ ” Lakini akajibu, “La! Nitafia hapa hapa.” Benaya akamwarifu mfalme, “Hivi ndivyo Yoabu alivyonijibu.”
31
Kisha mfalme akamwamuru Benaya, “Fanya kama asemavyo. Muue na kumzika, ili uniondolee mimi na nyumba ya baba yangu dhambi ya damu isiyokuwa na hatia ile Yoabu aliyoimwaga.
32
Bwana atamlipiza kwa ajili ya damu aliyoimwaga, kwa sababu pasipo Daudi baba yangu kujua, aliwashambulia watu wawili na kuwaua kwa upanga. Wote wawili, Abneri mwana wa Neri, jemadari wa jeshi la Israeli, na Amasa mwana wa Yetheri, jemadari wa jeshi la Yuda, walikuwa watu wazuri na wanyofu kuliko yeye.
33
Hatia ya damu yao na iwe juu ya kichwa cha Yoabu na wazao wake milele. Lakini kwa Daudi na uzao wake, nyumba yake na kiti chake cha ufalme, iwepo amani ya Bwana milele.”
34
Basi Benaya mwana wa Yehoyada akakwea, akampiga na kumuua Yoabu, naye akazikwa katika nchi yake mwenyewe katika jangwa.
35
Mfalme akamweka Benaya mwana wa Yehoyada juu ya jeshi kwenye nafasi ya Yoabu na kumweka kuhani Sadoki badala ya Abiathari.
36
Kisha mfalme akatuma ujumbe kwa Shimei na kumwambia, “Ujijengee nyumba huko Yerusalemu uishi huko, lakini usiende mahali pengine popote.
37
Siku utakayoondoka kuvuka Bonde la Kidroni, uwe na hakika utakufa; damu yako itakuwa juu ya kichwa chako mwenyewe.”
38
Shimei akamjibu mfalme, “Ulilolisema ni jema. Mtumishi wako atatenda kama bwana wangu mfalme alivyosema.” Naye Shimei akakaa Yerusalemu kwa muda mrefu.
39
Lakini baada ya miaka mitatu, watumwa wawili wa Shimei wakatoroka kwenda kwa Akishi mwana wa Maaka, mfalme wa Gathi, naye Shimei akaambiwa, “Watumwa wako wako Gathi.”
40
Kwa ajili ya hili, Shimei akatandika punda wake, akaenda kwa Akishi huko Gathi kuwatafuta watumwa wake. Basi Shimei akaondoka na kuwarudisha watumwa wake kutoka Gathi.
41
Solomoni alipoambiwa kuwa Shimei ametoka Yerusalemu na kwenda Gathi na amekwisha kurudi,
42
mfalme akamwita Shimei na kumwambia, “Je, sikukuapiza kwa Bwana na kukuonya kuwa, ‘Siku utakayoondoka kwenda mahali pengine popote, uwe na hakika utakufa?’ Wakati ule uliniambia, ‘Ulilolisema ni jema. Nitatii!’
43
Kwa nini basi hukutunza kiapo chako kwa Bwana na kutii amri niliyokupa?”
44
Pia mfalme akamwambia Shimei, “Unajua katika moyo wako makosa uliyomtendea baba yangu Daudi. Sasa Bwana atakulipiza kwa ajili ya mabaya yako uliyotenda.
45
Lakini Mfalme Solomoni atabarikiwa, na kiti cha ufalme cha Daudi kitakuwa imara mbele za Bwana milele.”
46
Kisha mfalme akatoa amri kwa Benaya mwana wa Yehoyada, naye akatoka nje, akampiga Shimei na kumuua. Sasa ufalme ukawa umeimarika kikamilifu mikononi mwa Solomoni.
Settings