1 Wafalme 15:16-34
16
Kulikuwa na vita kati ya Asa na Baasha mfalme wa Israeli siku zote za utawala wao.
17
Mfalme Baasha wa Israeli akashambulia Yuda na kuweka ngome mji wa Rama ili kumzuia yeyote asitoke wala kuingia nchi ya Mfalme Asa wa Yuda.
18
Kisha Asa akachukua fedha yote na dhahabu iliyokuwa imeachwa katika hazina za Hekalu la Bwana na za jumba lake mwenyewe la kifalme. Akawakabidhi maafisa wake na kuwatuma kwa Ben-Hadadi mwana wa Tabrimoni, mwana wa Hezioni, mfalme wa Aramu, aliyekuwa akitawala Dameski.
19
“Akasema na pawepo mkataba kati yangu na wewe, kama ulivyokuwepo kati ya baba yangu na baba yako. Tazama, nimekuletea zawadi ya fedha na dhahabu. Sasa vunja mkataba wako na Baasha mfalme wa Israeli ili aniondokee mimi.”
20
Ben-Hadadi akakubaliana na Mfalme Asa na kutuma majemadari wa majeshi yake dhidi ya miji ya Israeli. Akaishinda miji ya Iyoni, Dani, Abel-Beth-Maaka na Kinerethi yote, pamoja na Naftali.
21
Wakati Baasha aliposikia hili, akaacha kuijenga Rama na akaenda kuishi Tirsa.
22
Kisha Mfalme Asa akatoa amri kwa Yuda yote, pasipo kumbagua hata mmoja, kubeba mawe na mbao kutoka Rama, ambazo Baasha alikuwa akitumia huko. Mfalme Asa akazitumia kujengea Geba iliyoko Benyamini na Mispa pia.
23
Kwa matukio yote ya utawala wa Asa, mafanikio yake yote, yote aliyofanya na miji aliyoijenga, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? Katika uzee wake, hata hivyo, alipata ugonjwa wa miguu.
24
Kisha Asa akalala pamoja na baba zake na kuzikwa pamoja nao katika mji wa Daudi baba yake. Naye Yehoshafati mwanawe akawa mfalme baada yake.
25
Nadabu mwana wa Yeroboamu akawa mfalme wa Israeli katika mwaka wa pili wa utawala wa Mfalme Asa wa Yuda, naye akatawala Israeli kwa miaka miwili.
26
Akafanya maovu machoni pa Bwana, akienenda katika njia za baba yake na katika dhambi yake, ambayo alisababisha Israeli kuifanya.
27
Baasha mwana wa Ahiya wa nyumba ya Isakari akafanya shauri baya dhidi yake, naye akamuua huko Gibethoni, mji wa Wafilisti, wakati Nadabu na Israeli yote walipokuwa wameuzingira.
28
Baasha akamuua Nadabu katika mwaka wa tatu wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, naye Baasha akaingia mahali pake kuwa mfalme.
29
Mara tu alipoanza kutawala, aliua jamaa yote ya Yeroboamu. Hakumwachia Yeroboamu yeyote aliyekuwa hai, bali aliwaangamiza wote, kulingana na neno la Bwana lililotolewa kupitia kwa mtumishi wake Ahiya Mshiloni,
30
kwa sababu ya dhambi alizokuwa amezitenda Yeroboamu na kusababisha Israeli kuzitenda, tena kwa sababu alimkasirisha Bwana, Mungu wa Israeli.
31
Kwa matukio mengine ya utawala wa Nadabu na yote aliyofanya, je hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli?
32
Kulikuwa na vita kati ya Asa na Baasha mfalme wa Israeli wakati wote wa utawala wao.
33
Katika mwaka wa tatu wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, Baasha mwana wa Ahiya akawa mfalme wa Israeli yote huko Tirsa, naye akatawala kwa miaka ishirini na minne.
34
Akatenda maovu machoni pa Bwana, akienenda katika njia za Yeroboamu na dhambi yake, ambayo alikuwa amesababisha Israeli kuitenda.
Settings