Skip to content
Hesabu 11:18-34

Hesabu 11:18-34

18
“Waambie hao watu: ‘Jiwekeni wakfu wenyewe kwa ajili ya kesho, wakati mtakapokula nyama. Bwana aliwasikia mlipolia, mkisema, “Laiti tungekuwa na nyama tule! Tulikuwa na hali nzuri zaidi katika nchi ya Misri!” Sasa Bwana atawapa nyama, nanyi mtaila.
19
Hamtaila kwa siku moja tu, au siku mbili, au tano, kumi au siku ishirini,
20
bali kwa mwezi mzima mpaka iwatokee puani, nanyi mtaichukia kabisa, kwa kuwa mmemkataa Bwana, ambaye yupo miongoni mwenu, nanyi mmelia mbele zake, mkisema, “Hivi kwa nini tulitoka Misri?” ’ ”
21
Lakini Mose alisema, “Mimi niko hapa miongoni mwa watu 600,000 wanaotembea kwa miguu, nawe umesema, ‘Nitawapa nyama ya kula kwa mwezi mzima!’
22
Je, wangeweza kupata nyama ya kuwatosha hata kama makundi ya kondoo na ya ngʼombe yangechinjwa kwa ajili yao? Je, wangetosheka hata kama samaki wote wa baharini wangevuliwa kwa ajili yao?”
23
Bwana akamjibu Mose, “Je, mkono wa Bwana ni mfupi sana? Sasa utaona kama jambo nililolisema litatimizwa kwa ajili yako au la.”
24
Kwa hiyo Mose akatoka na kuwaambia watu lile ambalo Bwana alikuwa amesema. Akawakusanya wazee wao sabini, akawasimamisha kuzunguka Hema.
25
Kisha Bwana akashuka katika wingu na kunena na Mose, naye akachukua sehemu ya Roho iliyokuwa juu ya Mose na kuiweka juu ya wale wazee sabini. Roho aliposhuka juu yao, wakatoa unabii, lakini hawakufanya hivyo tena.
26
Lakini, watu wawili, ambao majina yao ni Eldadi na Medadi, walibaki kambini. Walikuwa wameorodheshwa miongoni mwa wale wazee sabini, lakini hawakutoka kwenda kwenye Hema. Lakini Roho pia alishuka juu yao, nao wakatabiri huko kambini.
27
Mwanaume mmoja kijana alikimbia na kumwambia Mose, “Eldadi na Medadi wanatoa unabii kambini.”
28
Yoshua mwana wa Nuni, ambaye alikuwa msaidizi wa Mose tangu ujana wake, akajibu akasema, “Mose bwana wangu, wanyamazishe!”
29
Lakini Mose akajibu, “Je, unaona wivu kwa ajili yangu? Ningetamani watu wote wa Bwana wangekuwa manabii na kwamba Bwana angeweka Roho yake juu yao!”
30
Ndipo Mose na wale wazee wa Israeli wakarudi kambini.
31
Kisha ukatokea upepo kutoka kwa Bwana, nao ukawaletea kware kutoka baharini. Ukawaangusha kwenye eneo lote linalozunguka kambi na kujaa ardhini kimo cha mita moja hivi kutoka ardhini kwenye eneo la umbali wa mwendo wa siku moja kila upande.
32
Mchana kutwa na usiku kucha pamoja na siku nzima iliyofuata watu walitoka kwenda kuokota kware. Hakuna mtu yeyote aliyekusanya chini ya homeri kumi. Kisha wakazianika kuzunguka kambi yote.
33
Lakini walipokuwa wakila nyama, ilipokuwa ingali kati ya meno yao na kabla hawajamaliza kula, hasira ya Bwana ikawaka dhidi ya watu, naye akawapiga kwa tauni.
34
Kwa hiyo mahali hapo pakaitwa Kibroth-Hataava, kwa sababu huko ndiko walipowazika watu ambao walitamani sana chakula kingine.
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Options