Marko 14:41-65
41
Akaja mara ya tatu, akawaambia, “Bado mmelala na kupumzika? Imetosha! Saa imewadia. Tazameni, Mwana wa Adamu anasalitiwa na kutiwa mikononi mwa wenye dhambi.
42
Inukeni, twende zetu! Tazameni, msaliti wangu yuaja!”
43
Yesu alipokuwa bado anazungumza, Yuda, mmoja wa wale wanafunzi Kumi na Wawili, akatokea. Alikuwa amefuatana na umati wa watu wenye panga na marungu, waliokuwa wametumwa na viongozi wa makuhani, walimu wa sheria, na wazee.
44
Basi msaliti alikuwa amewapa hao watu ishara, kwamba: “Yule nitakayembusu ndiye. Mkamateni, mkamchukue chini ya ulinzi.”
45
Mara Yuda akamjia Yesu na kusema, “Rabi.” Akambusu.
46
Wale watu wakamkamata Yesu, wakamweka chini ya ulinzi.
47
Ndipo mmoja wa wale waliokuwa wamesimama karibu aliuchomoa upanga wake na kumpiga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio.
48
Kisha Yesu akawaambia, “Mmekuja na panga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyangʼanyi?
49
Siku kwa siku nilikuwa pamoja nanyi nikifundisha Hekaluni, wala hamkunikamata. Lakini Maandiko sharti yatimie.”
50
Ndipo wanafunzi wake wote wakamwacha, wakakimbia.
51
Kijana mmoja, ambaye hakuwa amevaa kitu isipokuwa alijitanda nguo ya kitani, alikuwa akimfuata Yesu. Walipomkamata,
52
alikimbia uchi, akaliacha vazi lake.
53
Wakampeleka Yesu kwa kuhani mkuu, nao viongozi wa makuhani wote, na wazee na walimu wa sheria wote wakakusanyika pamoja.
54
Petro akamfuata kwa mbali, hadi uani kwa kuhani mkuu. Huko akaketi pamoja na walinzi, akiota moto.
55
Viongozi wa makuhani na Baraza la Wayahudi lote wakatafuta ushahidi dhidi ya Yesu ili wapate kumuua. Lakini hawakupata jambo lolote.
56
Wengi walitoa ushahidi wa uongo dhidi yake, lakini maelezo yao hayakukubaliana.
57
Ndipo wengine wakasimama wakatoa ushahidi wa uongo dhidi yake, wakisema:
58
“Sisi tulimsikia akisema, ‘Mimi nitalibomoa Hekalu hili lililojengwa na wanadamu, na katika siku tatu nitajenga jingine ambalo halikujengwa na wanadamu.’ ”
59
Lakini hata hivyo, ushahidi wao haukukubaliana.
60
Basi kuhani mkuu akasimama mbele yao, akamuuliza Yesu, “Je, wewe hutajibu? Ni ushahidi gani hawa watu wanauleta dhidi yako?”
61
Lakini Yesu akakaa kimya, hakusema neno lolote. Kuhani mkuu akamuuliza tena, “Je, wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu Aliyebarikiwa?”
62
Yesu akajibu, “Mimi ndimi. Nanyi mtamwona Mwana wa Adamu akiwa ameketi mkono wa kuume wa Mwenye Nguvu, na akija juu ya mawingu ya mbinguni.”
63
Kuhani mkuu akararua mavazi yake, akasema, “Tuna haja gani tena ya mashahidi zaidi?
64
Ninyi mmesikia hayo makufuru. Uamuzi wenu ni gani?” Wote wakamhukumu kwamba anastahili kifo.
65
Kisha baadhi ya watu wakaanza kumtemea mate; wakamfunga kitambaa machoni, wakampiga kwa ngumi na kumwambia, “Tabiri!” Walinzi wakamchukua na kumpiga makofi.
Settings