Skip to content
Waamuzi 7:1-15

Waamuzi 7:1-15

1
Ndipo Yerub-Baali (yaani Gideoni) na lile jeshi lililokuwa pamoja naye, wakaondoka asubuhi na mapema na kupiga kambi kando ya chemchemi ya Harodi. Kambi ya Wamidiani ilikuwa kaskazini yao katika bonde karibu na kilima cha More.
2
Bwana akamwambia Gideoni, “Jeshi lililo pamoja nawe ni kubwa sana kwa mimi kuwatia Wamidiani mikononi mwao. Ili kwamba Israeli asije akajisifu juu yangu akisema, ‘Mkono wangu ndio ulioniokoa,
3
kwa hiyo sasa tangaza jeshi lote likiwa linasikia, kwamba: Yeyote anayeogopa na kutetemeka, yeye na arudi nyumbani, aondoke katika Mlima Gileadi.’ ” Hivyo watu 22,000 walirudi, wakabaki 10,000.
4
Lakini Bwana akamwambia Gideoni, “Idadi ya jeshi bado ni kubwa. Wapeleke chini katika maji nami nitawajaribu huko kwa ajili yako. Kama nikikuambia, ‘Huyu atakwenda pamoja nawe,’ yeye atakwenda; lakini kama nikisema, ‘Huyu hatakwenda pamoja nawe,’ yeye hatakwenda.”
5
Hivyo Gideoni akalileta lile jeshi chini kwenye maji naye Bwana akamwambia Gideoni, “Watenge upande mmoja wale wote wanywao maji kwa ulimi, kama vile mbwa anywavyo, wale wote wapigao magoti ili kunywa wakipeleka mikono yao vinywani mwao, waweke upande mwingine.”
6
Idadi ya wale waliokunywa kwa kuramba ramba walikuwa 300, lakini wengine wote katika jeshi walipiga magoti ili kunywa.
7
Bwana akamwambia Gideoni, “Kwa hao watu 300 walioramba maji nitawaokoa ninyi, nami nitawatia Wamidiani mkononi mwako. Waache hao watu wengine wote warudi kila mmoja nyumbani mwake.”
8
Hivyo Gideoni akawaacha wale Waisraeli wengine kila mmoja aende kwenye hema yake. Akabakia na wale 300, ambao walichukua vyakula na tarumbeta za wale wenzao. Basi kambi ya Wamidiani ilikuwa chini yake bondeni.
9
Usiku ule ule Bwana akamwambia Gideoni, “Ondoka, ushuke kambini, kwa kuwa nimeitia mkononi mwako.
10
Lakini kama unaogopa kushambulia, shuka kambini pamoja na mtumishi wako Pura,
11
nawe sikiliza wanayosema. Hatimaye, utatiwa moyo kushambulia kambi.” Basi yeye na Pura mtumishi wake wakashuka na kufikia walinzi wa mbele wenye silaha waliokuwa mle kambini.
12
Wamidiani, Waamaleki na mataifa mengine yote ya mashariki walikaa bondeni, nao walikuwa mfano wa nzige kwa wingi wao. Ngamia zao hazikuhesabika, wingi wao ulikuwa kama mchanga wa ufuoni mwa bahari.
13
Gideoni alifika wakati huo huo kukiwa na mtu mmoja aliyekuwa anamweleza mwenzake ndoto yake, akisema, “Niliota ndoto: Tazama mkate wa shayiri ulioviringana ulianguka katika kambi moja ya Wamidiani, ukaipiga na ikaanguka nao ukaipindua juu chini na hema ikaporomoka chini.”
14
Rafiki yake akamjibu, “Habari hii si kitu kingine zaidi ya upanga wa Gideoni mwana wa Yoashi, Mwisraeli. Mungu amewatia Wamidiani na jeshi lote mkononi mwake.”
15
Gideoni alipoisikia hiyo ndoto na tafsiri yake, akamwabudu Mungu. Akarudi kwenye kambi ya Israeli na kusema, “Inukeni! Bwana amelitia jeshi la Wamidiani mikononi mwenu.”

Maandiko ya Biblia: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu)™, © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. · CC BY-SA 4.0“Biblica” is a trademark registered in the United States Patent and Trademark Office by Biblica, Inc., used with permission.

Settings

Reading style

Typeface

Font size 19px

Reading width 75 chars

Options