Mwanzo 33:8-20
8
Esau akauliza, “Una maana gani kuhusu makundi hayo yote niliyokutana nayo?” Akasema, “Ni ili kupata kibali machoni pako, bwana wangu.”
9
Lakini Esau akamwambia, “Ndugu yangu, tayari nina wingi wa mali. Ulivyo navyo viwe vyako mwenyewe.”
10
Yakobo akasema, “La hasha! Tafadhali, kama nimepata kibali machoni pako, upokee zawadi hii kutoka kwangu. Kwa maana kuuona uso wako, ni kama kuuona uso wa Mungu, kwa kuwa umenipokea kwa takabali kubwa.
11
Tafadhali ukubali zawadi iliyoletwa kwako, kwa kuwa Mungu amenineemesha na ninavyo vyote ninavyohitaji.” Kwa sababu Yakobo alisisitiza, Esau akapokea.
12
Ndipo Esau akasema, “Na tuendelee na safari, nitakuwa pamoja nawe.”
13
Lakini Yakobo akamwambia, “Bwana wangu unajua kwamba watoto ni wachanga na kwamba ni lazima nitunze hawa kondoo wake na ngʼombe wanaonyonyesha. Wakipelekwa kwa haraka hata kama ni kwa siku moja tu, wanyama wote watakufa.
14
Hivyo bwana wangu umtangulie mtumishi wako, wakati mimi nikija polepole kwa mwendo wa makundi yaliyo mbele yangu na mwendo wa watoto, mpaka nifike kwa bwana wangu huko Seiri.”
15
Esau akamwambia, “Basi na niwaache baadhi ya watu wangu pamoja nawe.” Yakobo akauliza, “Lakini kwa nini ufanye hivyo, niache tu nipate kibali machoni pa bwana wangu.”
16
Hivyo siku hiyo Esau akashika njia akarudi Seiri.
17
Pamoja na hayo, Yakobo akaenda Sukothi, mahali alipojijengea makazi kwa ajili yake na mabanda kwa ajili ya mifugo yake. Hii ndiyo sababu sehemu ile inaitwa Sukothi.
18
Baada ya Yakobo kutoka Padan-Aramu, alifika salama katika mji wa Shekemu huko Kanaani na kuweka kambi yake karibu na mji.
19
Akanunua kiwanja kutoka kwa wana wa Hamori, baba wa Shekemu, kwa bei ya vipande mia vya fedha, ambapo alipiga hema lake.
20
Pale akajenga madhabahu na kupaita El-Elohe-Israeli.
Maandiko ya Biblia: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu)™, © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. · CC BY-SA 4.0“Biblica” is a trademark registered in the United States Patent and Trademark Office by Biblica, Inc., used with permission.
Settings