Mwanzo 30:1-24
1
Raheli alipoona hamzalii Yakobo watoto, akamwonea ndugu yake wivu. Hivyo akamwambia Yakobo, “Nipe watoto, la sivyo nitakufa!”
2
Yakobo akamkasirikia, akamwambia, “Je, mimi ni badala ya Mungu, ambaye amekuzuia usizae watoto?”
3
Ndipo Raheli akamwambia, “Hapa yupo Bilha, mtumishi wangu wa kike. Kutana naye kimwili ili aweze kunizalia watoto na kwa kupitia yeye mimi pia niweze kuwa na uzao.”
4
Hivyo Raheli akampa Yakobo Bilha awe mke wake. Yakobo akakutana naye kimwili,
5
Bilha akapata mimba, naye akamzalia Yakobo mwana.
6
Ndipo Raheli akasema, “Mungu amenipa haki yangu, amesikiliza maombi yangu na kunipa mwana.” Kwa sababu hiyo akamwita Dani.
7
Bilha mtumishi wa kike wa Raheli akapata mimba tena, akamzalia Yakobo mwana wa pili.
8
Ndipo Raheli akasema, “Nilikuwa na mashindano makubwa na ndugu yangu, nami nimeshinda.” Kwa hiyo akamwita Naftali.
9
Lea alipoona kuwa amekoma kuzaa watoto, alimchukua mtumishi wake wa kike Zilpa, naye akampa Yakobo awe mke wake.
10
Mtumishi wa Lea yaani Zilpa, akamzalia Yakobo mwana.
11
Ndipo Lea akasema, “Hii ni bahati nzuri aje!” Kwa hiyo akamwita Gadi.
12
Mtumishi wa kike wa Lea akamzalia Yakobo mwana wa pili.
13
Ndipo Lea aliposema, “Jinsi gani nilivyo na furaha! Wanawake wataniita furaha.” Kwa hiyo akamwita Asheri.
14
Wakati wa kuvuna ngano, Reubeni akaenda shambani akakuta tunguja, ambazo alizileta kwa Lea mama yake. Raheli akamwambia Lea, “Tafadhali nakuomba unipe baadhi ya tunguja za mwanao.”
15
Lakini Lea akamwambia, “Haikukutosha kumtwaa mume wangu? Je, utachukua na tunguja za mwanangu pia?” Raheli akasema, “Vema sana! Yakobo atakutana nawe kimwili leo usiku, kwa malipo ya tunguja za mwanao.”
16
Kwa hiyo Yakobo alipokuja kutoka shambani jioni ile, Lea akaenda kumlaki, akamwambia, “Lazima ukutane nami kimwili. Nimekukodisha kwa tunguja za mwanangu.” Kwa hiyo akakutana naye kimwili usiku ule.
17
Mungu akamsikiliza Lea, naye akapata mimba akamzalia Yakobo mwana wa tano.
18
Ndipo Lea akasema, “Mungu amenizawadia kwa kumpa mume wangu mtumishi wangu wa kike.” Kwa hiyo akamwita Isakari.
19
Lea akapata mimba tena akamzalia Yakobo mwana wa sita.
20
Ndipo Lea aliposema, “Mungu amenizawadia kwa zawadi ya thamani sana. Wakati huu mume wangu ataniheshimu kwa sababu nimemzalia wana sita.” Kwa hiyo akamwita Zabuloni.
21
Baadaye akamzaa mtoto wa kike akamwita Dina.
22
Ndipo Mungu akamkumbuka Raheli, akasikia maombi yake na akafungua tumbo lake.
23
Akapata mimba na akamzaa mwana na kusema, “Mungu ameniondolea aibu yangu.”
24
Akamwita Yosefu na kusema, “Bwana na anipe mwana mwingine.”
Settings