Mwanzo 18:1-24
1
Bwana akamtokea Abrahamu karibu na mialoni ya Mamre wakati alipokuwa ameketi kwenye ingilio la hema lake wakati wa adhuhuri.
2
Abrahamu akainua macho akaona watu watatu wamesimama karibu naye. Alipowaona, aliharakisha kutoka kwenye ingilio la hema lake kuwalaki na kuwasujudia hadi nchi.
3
Akasema, “Kama nimepata kibali machoni penu, ee bwana wangu, usimpite mtumishi wako.
4
Acha yaletwe maji kidogo, kisha ninyi nyote mnawe miguu yenu na mpumzike chini ya mti huu.
5
Niruhusuni niwapatie chakula kidogo mle, ili mpate nguvu mwendelee na safari yenu, kwa kuwa mmekuja kwa mtumishi wenu.” Nao wakamjibu, “Vema sana, fanya kama unavyosema.”
6
Hivyo Abrahamu akaharakisha akaingia hemani kwa Sara, akamwambia, “Chukua vipimo vitatu vya unga laini haraka, ukande na uoke mikate.”
7
Kisha Abrahamu akakimbia kwenda kwenye kundi, akachagua ndama mzuri, laini na akampa mtumishi, ambaye aliharakisha kumtayarisha.
8
Kisha akaleta jibini, maziwa na nyama ya yule ndama iliyoandaliwa, akaviweka mbele ya wageni. Walipokuwa wakila, alisimama karibu nao chini ya mti.
9
Wakamuuliza, “Yuko wapi Sara mkeo?” Akasema, “Yuko huko, ndani ya hema.”
10
Kisha Bwana akasema, “Hakika nitakurudia tena majira kama haya mwakani na Sara mkeo atakuwa ana mwana.” Sara alikuwa akiwasikiliza kwenye ingilio la hema, lililokuwa nyuma yake.
11
Abrahamu na Sara walikuwa wazee tena waliosogea miaka, naye Sara alikuwa amekoma katika desturi ya wanawake.
12
Hivyo Sara akacheka kimoyomoyo alipokuwa akiwaza, “Baada ya mimi kuwa mkongwe hivi na bwana wangu amezeeka, je, nitaweza kufurahia jambo hili?”
13
Ndipo Bwana akamwambia Abrahamu, “Kwa nini Sara amecheka na kusema, ‘Kweli nitazaa mtoto nami sasa ni mzee?’
14
Je, kuna jambo lolote gumu lisilowezekana kwa Bwana? Nitakurudia mwakani majira kama haya, naye Sara atakuwa na mwana.”
15
Sara akaogopa kwa kuwa alidanganya na kusema, “Mimi sikucheka.” Lakini Bwana akasema, “Ndiyo, ulicheka!”
16
Wakati watu hao waliposimama ili waondoke, walielekeza nyuso zao Sodoma, Abrahamu akawatoa kitambo kidogo ili awasindikize.
17
Ndipo Bwana akasema, “Je, nimfiche Abrahamu jambo ninalokusudia kufanya?
18
Hakika Abrahamu atakuwa taifa kubwa na lenye nguvu, kupitia kwake mataifa yote ya dunia yatabarikiwa.
19
Kwa maana nimemchagua yeye, ili awaongoze watoto wake na jamaa yake kufuata njia ya Bwana, kwa kuwa waadilifu na kutenda haki, ili Bwana atimize ahadi yake kwa Abrahamu.”
20
Basi Bwana akasema, “Kilio dhidi ya Sodoma na Gomora ni kikubwa sana na dhambi yao inasikitisha sana,
21
kwamba nitashuka nione kama waliyoyatenda ni mabaya kiasi cha kilio kilichonifikia. Kama sivyo, nitajua.”
22
Basi wale watu wakageuka wakaenda kuelekea Sodoma, lakini Abrahamu akabaki amesimama mbele za Bwana.
23
Ndipo Abrahamu akamsogelea akasema: “Je, utawaangamiza wenye haki na waovu?
24
Je, ikiwa watakuwepo watu wenye haki hamsini katika mji huo, hivi kweli utauangamiza na wala hutauacha kwa ajili ya hao watu hamsini wenye haki waliomo ndani yake?
Maandiko ya Biblia: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu)™, © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. · CC BY-SA 4.0“Biblica” is a trademark registered in the United States Patent and Trademark Office by Biblica, Inc., used with permission.
Settings