Ezekieli 40:6-23
6
Kisha akaenda kwenye lango linaloelekea mashariki. Akapanda ngazi zake akapima kizingiti cha lango, nacho kilikuwa na kina cha huo ufito.
7
Vyumba vya kupumzikia vya walinzi vilikuwa na urefu wa huo ufito mmoja na upana wa huo ufito, kuta zilizogawa vyumba hivyo vya mapumziko zilikuwa na unene wa dhiraa tano. Nacho kizingiti cha lango lililokuwa karibu na ukumbi unaoelekea hekaluni ulikuwa na kina cha huo ufito.
8
Kisha akapima baraza ya njia ya lango,
9
ambayo ilikuwa na kina cha dhiraa nane na miimo yake ilikuwa na unene wa dhiraa mbili. Baraza ya lango ilielekea Hekalu.
10
Ndani ya lango la mashariki kulikuwepo vyumba vitatu vya kupumzikia kila upande, vyote vitatu vilikuwa na vipimo vilivyo sawa, nazo nyuso za kuta zilizotenganisha kila upande zilikuwa na vipimo vilivyo sawa.
11
Kisha akapima upana wa ingilio la lango, ilikuwa dhiraa kumi na urefu wake ulikuwa dhiraa kumi na tatu.
12
Mbele ya kila chumba cha kupumzikia kulikuwepo ukuta uliokuwa na kimo cha dhiraa moja kwenda juu, navyo hivyo vyumba vilikuwa dhiraa sita mraba.
13
Kisha akapima njia ya lango kuanzia juu ya ukuta wa nyuma wa chumba kimoja cha kupumzikia hadi juu ya ukuta wa nyuma wa chumba upande wa pili; kukawa na nafasi ya dhiraa ishirini na tano kuanzia lango la ukuta mmoja hadi lango la ukuta uliokuwa upande mwingine.
14
Akapima pia ukumbi, urefu wa dhiraa ishirini na lango linalofuatia hiyo nguzo kila upande wa huo ukumbi.
15
Umbali kuanzia ingilio la njia ya lango hadi mwisho kabisa wa baraza yake ulikuwa dhiraa hamsini.
16
Kulikuwa na vidirisha kwenye hivyo vyumba vya walinzi na nguzo za hivyo vyumba zilikuwa kwenye mzunguko wa hilo lango, vivyo hivyo kulikuwa na madirisha yaliyozunguka kuelekeana na ua na juu ya kila nguzo kulikuwa na mapambo ya miti ya mitende.
17
Kisha akanileta katika ukumbi wa nje. Huko nikaona vyumba vingine pamoja na njia iliyokuwa imejengwa kuzunguka ukumbi wote, kulikuwa na vyumba thelathini vimepangana kando ya hiyo njia.
18
Njia hii iliyojengwa iliambaa na lango, ikiwa na urefu sawa na lango, hii ilikuwa ni njia ya chini.
19
Kisha akapima umbali kutoka ndani ya lango la chini mpaka nje ya ukumbi wa ndani, nao ulikuwa dhiraa mia moja upande wa mashariki na dhiraa mia moja upande wa kaskazini.
20
Kisha akapima urefu na upana wa lango linaloelekea kaskazini, kukabili ukumbi wa nje.
21
Vyumba vyake vilikuwa vitatu kila upande, kuta zilizogawanya vyumba na baraza ilikuwa na vipimo sawa na zile kuta za lango la kwanza. Zilikuwa na urefu wa dhiraa hamsini na upana wa dhiraa ishirini na tano.
22
Madirisha yake, baraza yake na nakshi yake ya miti ya mitende vilikuwa na vipimo sawasawa na vile vya lango linaloelekea mashariki. Kulikuwa na ngazi saba za kupandia huko, pamoja na baraza yake mkabala nazo.
23
Kulikuwa na lango kwenye ukumbi wa ndani lililoelekea lile lango la kaskazini, kama vile ilivyokuwa ule upande wa mashariki. Akapima kutoka lango moja hadi lile lililo mkabala nalo, lilikuwa dhiraa mia moja.
Settings