Ezekieli 16:1-26
1
Neno la Bwana likanijia kusema:
2
“Mwanadamu, ijulishe Yerusalemu kuhusu mwenendo wake wa machukizo
3
na useme, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi, analomwambia Yerusalemu: Wewe asili yako na kuzaliwa kwako ni katika nchi ya Kanaani, baba yako alikuwa Mwamori, naye mama yako alikuwa Mhiti.
4
Siku uliyozaliwa kitovu chako hakikukatwa, wala hukuogeshwa kwa maji ili kukufanya safi, wala hukusuguliwa kwa chumvi wala kufunikwa kwa nguo.
5
Hakuna yeyote aliyekuonea huruma au kukusikitikia kiasi cha kukutendea mojawapo ya mambo haya. Badala yake, ulipozaliwa ulitupwa nje penye uwanja, kwa kuwa katika siku uliyozaliwa ulidharauliwa.
6
“ ‘Ndipo nilipopita karibu nawe nikakuona ukigaagaa kwenye damu yako, nawe ulipokuwa umelala hapo penye hiyo damu nikakuambia, “Ishi!”
7
Nilikufanya uote kama mmea wa shambani. Ukakua na kuongezeka sana, ukawa kito cha thamani kuliko vyote. Matiti yako yakatokeza na nywele zako zikaota, wewe uliyekuwa uchi na bila kitu chochote.
8
“ ‘Baadaye nikapita karibu nawe, nilipokutazama na kukuona kuwa umefikia umri wa kupendwa, nililitandaza vazi langu juu yako na kuufunika uchi wako. Nikakuapia na kuingia kwenye Agano na wewe, asema Bwana Mwenyezi, nawe ukawa wangu.
9
“ ‘Nilikuogesha kwa maji, nikakuosha ile damu na kukupaka mafuta.
10
Nikakuvika vazi lililotariziwa na kukuvalisha viatu vya kamba vya ngozi. Nikakuvika nguo za kitani safi na kukufunika kwa mavazi ya thamani kubwa.
11
Nikakupamba kwa vito: nikakuvika bangili mikononi mwako na mkufu shingoni mwako,
12
nikaweka hazama puani mwako, vipuli masikioni mwako na taji nzuri sana kichwani mwako.
13
Kwa hiyo ulipambwa kwa dhahabu na fedha, nguo zako zilikuwa za kitani safi, hariri na nguo iliyokuwa imetariziwa. Chakula chako kilikuwa unga laini, asali na mafuta ya zeituni. Ukawa mzuri sana ukainuka kuwa malkia.
14
Umaarufu wako ulifahamika miongoni mwa mataifa kwa ajili ya uzuri wako, kwani ulikuwa mkamilifu kwa ajili ya utukufu wangu niliokuwa nimeuweka juu yako, asema Bwana Mwenyezi.
15
“ ‘Lakini ulitumainia uzuri wako na kutumia umaarufu wako kuwa kahaba. Ulifanya uzinzi kwa kila mtu aliyepita, uzuri wako ukawa kwa ajili yake.
16
Ulichukua baadhi ya mavazi yako ukayatumia kupamba mahali pako pa juu pa kuabudia miungu, mahali ambapo ulifanyia ukahaba wako. Mambo ya namna hiyo hayastahili kutendeka wala kamwe kutokea.
17
Pia ulichukua vito vizuri nilivyokupa, vito vilivyotengenezwa kwa dhahabu yangu na fedha yangu, ukajitengenezea navyo sanamu za kiume na ukafanya ukahaba nazo.
18
Ukayachukua mavazi yako niliyokupa yaliyotariziwa na ukazivalisha hizo sanamu, ukatoa mbele ya hizo sanamu mafuta yangu na uvumba wangu.
19
Pia chakula changu nilichokupa ili ule: unga laini, mafuta ya zeituni na asali, ulivitoa mbele yao kuwa uvumba wa harufu nzuri. Hayo ndiyo yaliyotokea, asema Bwana Mwenyezi.
20
“ ‘Nawe uliwachukua wanao na binti zako ulionizalia mimi na kuwatoa kafara kuwa chakula kwa sanamu. Je, ukahaba wako haukukutosha?
21
Uliwachinja watoto wangu na kuwatoa kafara kwa sanamu.
22
Katika matendo yako yote ya machukizo, pamoja na ukahaba wako hukukumbuka siku za ujana wako, wakati ulipokuwa uchi kabisa bila kitu chochote, ulipokuwa ukigaagaa kwenye damu yako.
23
“ ‘Ole! Ole wako! Asema Bwana Mwenyezi. Pamoja na maovu yako yote mengine,
24
Ukajijengea jukwaa na kujifanyia mahali pa fahari pa ibada za miungu kwenye kila uwanja wa mikutano.
25
Katika kila mwanzo wa barabara ulijenga mahali pa fahari pa ibada za miungu na kuaibisha uzuri wako, ukiutoa mwili wako kwa kuzidisha uzinzi kwa kila apitaye.
26
Ulifanya ukahaba wako na Wamisri, jirani zako waliojaa tamaa, ukaichochea hasira yangu kwa kuongezeka kwa uzinzi wako.
Settings