2 Nyakati 24:1-14
1
Yoashi alikuwa na umri wa miaka saba alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka arobaini. Mama yake aliitwa Sibia aliyekuwa ametoka Beer-Sheba.
2
Yoashi akafanya yaliyo mema machoni pa Bwana miaka yote ya Yehoyada kuhani.
3
Yehoyada akamwoza wake wawili, akazaa watoto wa kiume na wa kike.
4
Baada ya muda, Yoashi akaamua kukarabati Hekalu la Bwana.
5
Akawaita pamoja makuhani na Walawi akawaambia, “Nendeni katika miji ya Yuda mkakusanye fedha wanazopaswa kulipa kila mwaka kutoka kwa Israeli wote, ili kukarabati Hekalu la Mungu wenu. Fanyeni hivyo sasa.” Lakini Walawi hawakufanya upesi.
6
Kwa hiyo mfalme akamwita Yehoyada kuhani mkuu na kumwambia, “Kwa nini hukuwaambia Walawi walete kutoka Yuda na Yerusalemu kodi iliyowekwa na Mose mtumishi wa Bwana pamoja na kusanyiko la Israeli kwa ajili ya Hema ya Ushuhuda?”
7
Kwa kuwa wana wa yule mwanamke mwovu Athalia, walikuwa wamevunja na kuingia katika Hekalu la Mungu, nao wakawa wamevitumia hata vile vitu vilivyowekwa wakfu kwa Bwana kwa mabaali.
8
Kwa amri ya mfalme, likatengenezwa kasha, nalo likawekwa nje kwenye lango la Hekalu la Bwana.
9
Tangazo likatolewa katika Yuda na Yerusalemu kwamba inapasa wamletee Bwana kodi ile ambayo Mose, mtumishi wa Bwana alikuwa amewaagiza Israeli huko jangwani.
10
Maafisa wote na watu wote wakaleta michango yao kwa furaha, wakaweka kwenye kasha mpaka likajaa.
11
Ikawa kila wakati kasha lilipoletwa ndani na Walawi kwa maafisa wa mfalme na kuona kwamba kuna kiasi kikubwa cha fedha, mwandishi wa mfalme na afisa wa kuhani mkuu walikuwa wanakuja na kumimina, kisha kulirudisha mahali pake. Walifanya hivi mara kwa mara, nao wakakusanya fedha nyingi sana.
12
Mfalme na Yehoyada wakawapa wale watu waliofanya kazi iliyotakiwa katika Hekalu la Bwana. Wakawaajiri waashi na maseremala ili kutengeneza Hekalu la Bwana, pia wafanyakazi za chuma na shaba ili kukarabati Hekalu la Bwana.
13
Watu walioshughulika na kazi walikuwa wenye bidii, nayo kazi ya kukarabati ikaendelea vizuri mikononi mwao. Wakalitengeneza upya Hekalu la Bwana likarudi katika hali yake ya awali na kuliimarisha.
14
Walipokamilisha kazi hiyo ya kukarabati, wakaleta fedha zilizobaki wakampa mfalme na Yehoyada, nao kwa hizo wakatengeneza vyombo kwa ajili ya Hekalu la Bwana: Vyombo kwa ajili ya huduma na kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, pia mabakuli na vitu vingine vya dhahabu na fedha. Wakati wote Yehoyada alipokuwa hai, sadaka za kuteketezwa zilitolewa wakati wote katika Hekalu la Bwana.
Settings