1 Samweli 20:33-42
33
Lakini Sauli akamtupia Yonathani mkuki wake kwa nguvu ili amuue. Hapo ndipo Yonathani alipotambua kwamba baba yake alikusudia kumuua Daudi.
34
Yonathani akainuka kutoka mezani kwa hasira kali. Siku ile ya pili ya mwezi hakula chakula, kwa kuwa alikuwa amehuzunishwa na vitendo vya aibu ambavyo baba yake alikuwa anamtendea Daudi.
35
Kesho yake asubuhi Yonathani alikwenda shambani kukutana na Daudi. Alikuwa amefuatana na mvulana mdogo,
36
naye Yonathani akamwambia yule mvulana, “Kimbia ukatafute mishale nitakayorusha.” Mvulana alipokuwa akikimbia, akarusha mishale mbele yake.
37
Yule mvulana alipofika mahali pale ambapo mshale wa Yonathani ulipokuwa umeanguka, Yonathani akamwita, “Je, mshale hauko mbele yako?”
38
Yonathani akampigia kelele, “Harakisha, nenda haraka! Usisimame!” Mvulana akaokota mshale na kurudi kwa bwana wake.
39
(Mvulana hakujua chochote juu ya hayo yote; Yonathani na Daudi tu ndio waliojua.)
40
Basi Yonathani akampa yule mvulana silaha zake na kumwambia, “Nenda, zirudishe mjini.”
41
Baada ya mvulana kwenda, Daudi akainuka kutoka upande wa kusini wa lile jiwe, naye akasujudu uso wake mpaka nchi mara tatu mbele ya Yonathani. Kisha kila mmoja akambusu mwenzake, wakalia pamoja. Lakini Daudi akalia zaidi.
42
Yonathani akamwambia Daudi, “Nenda kwa amani, kwa kuwa tumeapiana kiapo cha urafiki kati yetu kwa jina la Bwana, tukisema, ‘Bwana ndiye shahidi kati yako na mimi, na kati ya wazao wako na wazao wangu milele.’ ” Kisha Daudi akaondoka, naye Yonathani akarudi mjini.
Maandiko ya Biblia: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu)™, © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. · CC BY-SA 4.0“Biblica” is a trademark registered in the United States Patent and Trademark Office by Biblica, Inc., used with permission.
Settings