1 Samweli 17:45-58
45
Daudi akamwambia yule Mfilisti. “Wewe unanijia na upanga, mkuki na fumo, lakini mimi ninakujia kwa jina la Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa majeshi ya Israeli, ambaye wewe umemtukana.
46
Siku hii leo Bwana atakutia mkononi mwangu, nami nitakupiga na kukukata kichwa chako. Leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya jeshi la Wafilisti, nayo dunia yote itajua kuwa yuko Mungu katika Israeli.
47
Wale wote waliokusanyika hapa watajua kuwa Bwana haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; kwa kuwa vita ni vya Bwana, naye atawatia wote mikononi mwetu.”
48
Yule Mfilisti aliposogea karibu ili kumshambulia, Daudi akaenda mbio kuelekea safu ya vita kukutana naye.
49
Daudi akatia mkono wake mfukoni na kuchukua jiwe, akalirusha kwa kombeo, nalo likampiga yule Mfilisti kwenye paji la uso. Lile jiwe likaingia kipajini mwa uso, akaanguka chini kifudifudi.
50
Basi Daudi akamshinda huyo Mfilisti kwa kombeo na jiwe; bila kuwa na upanga mikononi mwake akampiga huyo Mfilisti na kumuua.
51
Daudi akakimbia na kusimama juu yake. Akaushika upanga wa huyo Mfilisti na kuuvuta toka kwenye ala yake. Baada ya kumuua, akakata kichwa chake kwa ule upanga. Wafilisti walipoona kuwa shujaa wao amekufa, wakageuka na kukimbia.
52
Ndipo watu wa Israeli na Yuda wakainuka kwenda mbele wakipiga kelele na kufuatia Wafilisti mpaka kwenye ingilio la Gathi kwenye malango ya Ekroni. Maiti zao zilitawanyika kando ya barabara ya Shaaraimu hadi Gathi na Ekroni.
53
Waisraeli waliporudi kutoka kuwafukuza Wafilisti, waliteka nyara kutoka kambi yao.
54
Daudi akachukua kichwa cha yule Mfilisti na kukileta Yerusalemu, naye akaweka silaha za huyo Mfilisti katika hema lake mwenyewe.
55
Sauli alipomwona Daudi anakwenda kukabiliana na huyo Mfilisti, alimwambia Abneri, jemadari wa jeshi, “Abneri, yule kijana ni mwana wa nani?” Abneri akajibu, “Hakika kama uishivyo, ee mfalme, mimi sifahamu.”
56
Mfalme akasema, “Uliza huyu kijana ni mwana wa nani.”
57
Mara Daudi aliporudi kutoka kumuua huyo Mfilisti, Abneri akamchukua na kumleta mbele ya Sauli. Daudi alikuwa bado anakishikilia kichwa cha yule Mfilisti.
58
Sauli akamuuliza, “Kijana, wewe ni mwana wa nani?” Daudi akasema, “Mimi ni mwana wa mtumishi wako Yese wa Bethlehemu.”
Maandiko ya Biblia: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu)™, © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. · CC BY-SA 4.0“Biblica” is a trademark registered in the United States Patent and Trademark Office by Biblica, Inc., used with permission.
Settings