Skip to content
1 Samweli 17:32-51

1 Samweli 17:32-51

32
Daudi akamwambia Sauli, “Mtu yeyote asife moyo kwa habari ya huyu Mfilisti; mtumishi wako atakwenda kupigana naye.”
33
Sauli akamjibu Daudi, “Wewe hutaweza kwenda kupigana dhidi ya huyu Mfilisti; wewe ni kijana tu, naye amekuwa mtu wa vita tangu ujana wake.”
34
Lakini Daudi akamwambia Sauli, “Mtumishi wako amekuwa akichunga kondoo wa baba yake. Wakati simba au dubu alikuja na kuchukua kondoo kutoka kundi,
35
nilifuatia, nikampiga na nikampokonya kondoo kwenye kinywa chake. Aliponigeukia, nilimkamata nywele zake, nikampiga na kumuua.
36
Mtumishi wako ameshaua simba na dubu pia; huyu Mfilisti asiyetahiriwa atakuwa kama mmoja wa hao, kwa sababu ameyatukana majeshi ya Mungu aliye hai.
37
Bwana ambaye aliniokoa toka katika makucha ya simba na makucha ya dubu ataniokoa kutoka mikono ya huyu Mfilisti.” Sauli akamwambia Daudi, “Nenda, naye Bwana na awe pamoja nawe.”
38
Ndipo Sauli akamvika Daudi silaha zake mwenyewe za vita. Akamvika dirii na chapeo ya shaba kichwani mwake.
39
Daudi akajifunga upanga juu ya hayo mavazi na kujaribu kutembea kwa sababu alikuwa hana uzoefu navyo. Daudi akamwambia Sauli, “Siwezi kwenda nikiwa nimevaa hivi, kwa sababu sina uzoefu navyo.” Hivyo akavivua.
40
Kisha akachukua fimbo yake mkononi, akachagua mawe laini matano kutoka kwenye kijito, akayaweka kwenye kifuko ndani ya mfuko wake wa kichungaji, akiwa na kombeo yake mkononi mwake, akamkaribia yule Mfilisti.
41
Wakati ule ule, yule Mfilisti, akiwa na mbeba ngao wake mbele yake, akaendelea kujongea karibu na Daudi.
42
Mfilisti akamwangalia Daudi kote na kumwona kuwa ni kijana tu, mwekundu na mzuri wa kupendeza, naye akamdharau.
43
Akamwambia Daudi, “Je, mimi ni mbwa, hata unanijia na fimbo?” Yule Mfilisti akamlaani Daudi kwa miungu yake.
44
Tena Mfilisti akamwambia, “Njoo hapa, nami nitawapa ndege wa angani na wanyama wa mwituni nyama yako.”
45
Daudi akamwambia yule Mfilisti. “Wewe unanijia na upanga, mkuki na fumo, lakini mimi ninakujia kwa jina la Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa majeshi ya Israeli, ambaye wewe umemtukana.
46
Siku hii leo Bwana atakutia mkononi mwangu, nami nitakupiga na kukukata kichwa chako. Leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya jeshi la Wafilisti, nayo dunia yote itajua kuwa yuko Mungu katika Israeli.
47
Wale wote waliokusanyika hapa watajua kuwa Bwana haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; kwa kuwa vita ni vya Bwana, naye atawatia wote mikononi mwetu.”
48
Yule Mfilisti aliposogea karibu ili kumshambulia, Daudi akaenda mbio kuelekea safu ya vita kukutana naye.
49
Daudi akatia mkono wake mfukoni na kuchukua jiwe, akalirusha kwa kombeo, nalo likampiga yule Mfilisti kwenye paji la uso. Lile jiwe likaingia kipajini mwa uso, akaanguka chini kifudifudi.
50
Basi Daudi akamshinda huyo Mfilisti kwa kombeo na jiwe; bila kuwa na upanga mikononi mwake akampiga huyo Mfilisti na kumuua.
51
Daudi akakimbia na kusimama juu yake. Akaushika upanga wa huyo Mfilisti na kuuvuta toka kwenye ala yake. Baada ya kumuua, akakata kichwa chake kwa ule upanga. Wafilisti walipoona kuwa shujaa wao amekufa, wakageuka na kukimbia.
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Options