1 Wafalme 16:9-20
9
Zimri, mmoja wa maafisa wake, aliyekuwa na amri juu ya nusu ya magari yake ya vita, akafanya hila mbaya dhidi ya Ela. Wakati huo Ela alikuwa Tirsa, akilewa katika nyumba ya Arsa, mtu aliyekuwa msimamizi wa jumba la kifalme huko Tirsa.
10
Zimri akaingia, akampiga na kumuua katika mwaka wa ishirini na saba wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda. Kisha Zimri akaingia mahali pake kuwa mfalme.
11
Mara tu alipoanza kutawala na kuketi juu ya kiti cha ufalme, aliua jamaa yote ya Baasha. Hakumwacha mwanaume hata mmoja, akiwa ni ndugu au rafiki.
12
Hivyo Zimri akaangamiza jamaa yote ya Baasha, kulingana na neno la Bwana lililonenwa dhidi ya Baasha kupitia nabii Yehu:
13
kwa sababu ya dhambi zote Baasha na mwanawe Ela walizokuwa wametenda na wakasababisha Israeli kuzitenda, basi wakamkasirisha Bwana, Mungu wa Israeli kwa sanamu zao zisizofaa.
14
Kwa matukio mengine ya utawala wa Ela, na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli?
15
Katika mwaka wa ishirini na saba wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, Zimri akatawala huko Tirsa siku saba. Jeshi lilikuwa limepiga kambi karibu na Gibethoni, mji wa Wafilisti.
16
Wakati Waisraeli waliokuwa kambini waliposikia kuwa Zimri alikuwa amefanya hila mbaya dhidi ya mfalme na kumuua, wakamtangaza Omri, jemadari wa jeshi, kuwa mfalme wa Israeli siku iyo hiyo huko kambini.
17
Ndipo Omri na Waisraeli wote pamoja naye wakaondoka Gibethoni na kuizingira Tirsa.
18
Wakati Zimri alipoona kuwa mji umechukuliwa, alikwenda ndani ya ngome ya jumba la kifalme na kulichoma moto jumba la kifalme na kujiteketeza ndani yake. Kwa hiyo akafa,
19
kwa sababu ya dhambi alizofanya, akitenda maovu machoni pa Bwana na kuenenda katika njia za Yeroboamu na katika dhambi alizofanya na kusababisha Israeli kuzifanya.
20
Kwa matukio mengine ya utawala wa Zimri, na uasi alioutenda, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli?
Settings