1 Nyakati 21:5-17
5
Yoabu akampa Daudi jumla ya idadi ya watu wanaoweza kupigana. Katika Israeli kulikuwa na watu 1,100,000 ambao wangeweza kutumia upanga na katika Yuda watu 470,000.
6
Lakini Yoabu hakuwahesabu Walawi na Wabenyamini, kwa sababu alichukizwa sana na amri ya mfalme.
7
Amri hii ilikuwa mbaya machoni pa Mungu pia; hivyo akaiadhibu Israeli.
8
Kisha Daudi akamwambia Mungu, “Nimetenda dhambi kubwa kwa kufanya jambo hili. Sasa, ninakusihi, ondoa hatia ya mtumishi wako. Nimefanya jambo la kipumbavu sana.”
9
Bwana akamwambia Gadi, mwonaji wa Daudi,
10
“Nenda ukamwambie Daudi, hivi ndivyo asemavyo Bwana: ‘Ninakupa wewe uchaguzi wa mambo matatu. Nichagulie mojawapo nitakalotenda dhidi yako.’ ”
11
Kwa hiyo Gadi akamwendea Daudi akamwambia, “Hili ndilo Bwana asemalo: ‘Chagua:
12
miaka mitatu ya njaa, au miezi mitatu ya kushindwa na adui zako, ukipatwa na upanga wao, au siku tatu za upanga wa Bwana, yaani, siku tatu za tauni katika nchi na malaika wa Bwana akiangamiza kila mahali katika Israeli.’ Sasa basi, amua jinsi nitakavyomjibu yeye aliyenituma.”
13
Daudi akamwambia Gadi, “Ninayo mahangaiko makubwa. Mimi na nianguke mikononi mwa Bwana kwa maana rehema zake ni kuu mno, lakini usiniache niangukie mikononi mwa wanadamu.”
14
Basi Bwana akatuma tauni katika Israeli, watu 70,000 wa Israeli wakafa.
15
Mungu akapeleka malaika kuangamiza Yerusalemu. Lakini malaika alipokuwa akifanya hivyo, Bwana akaona na akahuzunika kwa sababu ya maafa, akamwambia yule malaika aliyekuwa anaangamiza watu, “Yatosha! Rudisha mkono wako.” Wakati huo malaika wa Bwana alikuwa amesimama katika sakafu ya kupuria nafaka ya Arauna Myebusi.
16
Daudi akayainua macho yake akamwona huyo malaika wa Bwana akiwa amesimama katikati ya mbingu na dunia, naye ameunyoosha upanga wake juu ya Yerusalemu tayari kuangamiza. Kisha Daudi na wazee, waliokuwa wamevaa nguo za gunia, wakaanguka kifudifudi.
17
Daudi akamwambia Mungu, “Je, si mimi ndiye niliyeamuru watu wahesabiwe? Mimi ndiye niliyetenda dhambi na kukosa. Hawa ni kondoo tu. Wamefanya nini? Ee Bwana, Mungu wangu, mkono wako na uwe juu yangu mimi na jamaa yangu, lakini usiache tauni hii iendelee juu ya watu wako.”
Settings