1 Nyakati 12:23-40
23
Hawa ndio watu waliojiandaa kwa ajili ya vita waliokuja kwa Daudi huko Hebroni ili kumtwalia ufalme kutoka kwa Sauli, kama Bwana alivyokuwa amesema:
24
watu wa Yuda, wanaochukua ngao na mikuki walikuwa 6,800 wote wakiwa tayari kwa vita.
25
Watu wa Simeoni, mashujaa waliokuwa tayari kwa vita walikuwa 7,100.
26
Watu wa Lawi walikuwa 4,600,
27
pamoja na Yehoyada, kiongozi wa jamaa ya Aroni, aliyekuwa pamoja na watu 3,700,
28
na Sadoki, kijana shujaa na hodari, aliyekuwa pamoja na maafisa ishirini na wawili kutoka jamaa yake.
29
Watu wa Benyamini, ndugu zake Sauli, walikuwa 3,000; wengi wao walikuwa wameendelea kuwa waaminifu kwa Sauli mpaka wakati huo.
30
Watu wa Efraimu, mashujaa hodari 20,800, watu waliokuwa maarufu katika koo zao.
31
Watu wa nusu ya kabila la Manase, waliotajwa kwa majina ili waje kumweka Daudi kuwa mfalme, watu 18,000.
32
Watu wa Isakari, waliofahamu majira na kujua kile ambacho Israeli inapasa kufanya, walikuwa viongozi 200, pamoja na jamaa zao wote chini ya uongozi wao.
33
Watu wa Zabuloni, askari wenye uzoefu mkubwa walioandaliwa tayari kwa vita wakiwa na silaha za kila aina, ili kumsaidia Daudi kwa uaminifu thabiti, walikuwa 50,000.
34
Watu wa Naftali, maafisa 1,000, pamoja na watu 37,000 waliochukua ngao na mikuki.
35
Watu wa Dani 28,600 waliokuwa tayari kwa vita.
36
Watu wa Asheri, askari 40,000 wenye uzoefu mkubwa waliondaliwa kwa ajili ya vita.
37
Na pia watu kutoka mashariki ya Yordani, watu wa Reubeni, Gadi na nusu ya kabila la Manase, wakiwa na kila aina ya silaha, watu 120,000.
38
Wote hawa walikuwa watu wapiganaji waliojitolea kutumika katika safu zao. Walikuja Hebroni wakiwa wameamua kikamilifu kumfanya Daudi mfalme juu ya Israeli yote. Waisraeli wengine wote walikuwa pia na nia hiyo moja ya kumfanya Daudi kuwa mfalme.
39
Watu hawa wakakaa huko na Daudi siku tatu, wakila na kunywa, kwa sababu jamaa zao zilikuwa zimewapatia mahitaji yao.
40
Pia, majirani zao hata wale walio mbali hadi Isakari, Zabuloni na Naftali, walikuja wakiwaletea vyakula walivyovibeba kwa punda, ngamia, nyumbu na maksai. Kulikuwepo na wingi wa unga, maandazi ya tini, maandazi ya zabibu kavu, divai, mafuta, ngʼombe na kondoo, kwa maana kulikuwa na furaha katika Israeli.
Settings