1 Nyakati 12:1-22
1
Hawa ndio watu waliomjia Daudi huko Siklagi, wakati alikuwa amefukuzwa mbele ya Sauli mwana wa Kishi (walikuwa miongoni mwa mashujaa waliomsaidia Daudi vitani,
2
walikuwa na pinde na walikuwa na uwezo wa kupiga mishale au kutupa mawe kwa kombeo wakitumia mkono wa kushoto au wa kulia; hawa walikuwa ndugu zake Sauli kutoka kabila la Benyamini):
3
Mkuu wao alikuwa Ahiezeri, na wa pili Yoashi, wote wana wa Shemaa Mgibeathi; pia Yezieli na Peleti wana wa Azmawethi; Beraka, Yehu Mwanathothi,
4
na Ishmaya Mgibeoni, shujaa miongoni mwa wale Thelathini, ambaye alikuwa kiongozi wa wale Thelathini; Yeremia, Yahazieli, Yohanani, Yozabadi, Mgederathi,
5
Eluzai, Yeremothi, Bealia, Shemaria, Shefatia, Mharufi;
6
Elikana, Ishia, Azareli, Yoezeri na Yashobeamu, wana wa Kora;
7
Yoela na Zebadia, wana wa Yerohamu, kutoka Gedori.
8
Baadhi ya Wagadi wakajitenga na kujiunga na Daudi katika ngome yake huko jangwani. Walikuwa mashujaa hodari, waliokuwa tayari kwa vita na wenye uwezo wa kutumia ngao na mkuki. Nyuso zao zilikuwa nyuso za simba na walikuwa na wepesi kama paa milimani.
9
Ezeri alikuwa mkuu wao, Obadia alikuwa wa pili katika uongozi, Eliabu wa tatu,
10
Mishmana wa nne, Yeremia wa tano,
11
Atai wa sita, Elieli wa saba,
12
Yohanani wa nane, Elzabadi wa tisa,
13
Yeremia wa kumi, na Makbanai wa kumi na moja.
14
Hawa Wagadi walikuwa majemadari. Aliyekuwa wa mwisho kuliko wote aliweza kuongoza askari 100, na aliyekuwa na uweza zaidi ya wote aliongoza 1,000.
15
Wao ndio walivuka Mto Yordani katika mwezi wa kwanza ukiwa umefurika hadi kwenye kingo zake zote na kusababisha watu wote waliokuwa wanaishi kwenye mabonde kukimbilia mashariki na wengine magharibi.
16
Wabenyamini wengine na baadhi ya watu kutoka Yuda pia walikuja kwa Daudi katika ngome yake.
17
Daudi akatoka nje kuwalaki na akawaambia, “Kama mmekuja kwangu kwa amani, kunisaidia, mimi niko tayari kuwaruhusu ninyi kuungana nami. Lakini kama mmekuja ili kunisaliti kwa adui zangu wakati mimi mikono yangu haina hatia, basi Mungu wa baba zetu aone na awahukumu.”
18
Kisha Roho akaja juu ya Amasai, mkuu wa wale Thelathini, naye akasema: “Sisi tu watu wako, ee Daudi! Nasi tuko pamoja na wewe, ee mwana wa Yese! Ushindi, naam, ushindi uwe kwako, pia ushindi kwa wale walio upande wako, kwa kuwa Mungu wako atakusaidia.” Kwa hiyo Daudi akawapokea na kuwafanya viongozi wa vikosi vyake vya uvamizi.
19
Baadhi ya watu kutoka kabila la Manase wakajiunga na Daudi wakati alikwenda pamoja na Wafilisti, kupigana na Sauli. (Daudi na watu wake hawakuwasaidia Wafilisti kwa sababu, baada ya ushauri, watawala wao walimrudisha. Wakasema, “Itatugharimu vichwa vyetu kama Daudi atatuasi na kurudi kwa Sauli bwana wake.”)
20
Daudi alipokwenda Siklagi, hawa ndio watu wa kabila la Manase waliojiunga naye: Adna, Yozabadi, Yediaeli, Mikaeli, Yozabadi, Elihu na Silethai, viongozi wa vikosi vya watu 1,000 katika kabila la Manase.
21
Walimsaidia Daudi dhidi ya makundi ya uvamizi, kwa kuwa wote walikuwa mashujaa hodari na walikuwa majemadari katika jeshi lake.
22
Siku baada ya siku watu walikuja kumsaidia Daudi, mpaka akawa na jeshi kubwa, kama jeshi la Mungu.
Settings