Rukia maudhui

Mithali3

Ishike Sheria, Upate Kibali

1
Mwanangu, usisahau mafundisho yangu, bali zitunze amri zangu moyoni mwako,
2
kwa kuwa zitakuongezea miaka mingi ya maisha yako na kukuletea mafanikio.
3
Usiache kamwe upendo na uaminifu vitengane nawe; vifunge shingoni mwako, viandike katika ubao wa moyo wako.
4
Ndipo utapata kibali na jina zuri mbele za Mungu na mwanadamu.

Mtumaini BWANA kwa Moyo Wako Wote

5
Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote wala usizitegemee akili zako mwenyewe;
6
katika njia zako zote mkiri yeye, naye atayanyoosha mapito yako.
7
Usiwe mwenye hekima machoni pako mwenyewe; mche Bwana ukajiepushe na uovu.
8
Hii itakuletea afya mwilini mwako, na mafuta kwenye mifupa yako.

Mheshimu Mungu kwa Mali Yako

9
Mheshimu Bwana kwa mali zako na kwa malimbuko ya mazao yako yote;
10
ndipo ghala zako zitakapojaa hadi kufurika, viriba vyako vitafurika kwa mvinyo mpya.

Usidharau Nidhamu

11
Mwanangu, usiidharau adhabu ya Bwana na usichukie kukaripiwa naye,
12
kwa sababu Bwana huwaadibisha wale awapendao, kama vile baba afanyavyo kwa mwana apendezwaye naye.

Thamani ya Hekima Isiyopimika

13
Heri mtu yule aonaye hekima, mtu yule apataye ufahamu,
14
kwa maana hekima ana faida kuliko fedha na mapato yake ni bora kuliko ya dhahabu safi.
15
Hekima ana thamani kuliko marijani; hakuna chochote unachokitamani kinachoweza kulinganishwa naye.
16
Maisha marefu yako katika mkono wake wa kuume; katika mkono wake wa kushoto kuna utajiri na heshima.
17
Njia zake zinapendeza, mapito yake yote ni amani.
18
Yeye ni mti wa uzima kwa wale wanaomkumbatia; wale wamshikao watabarikiwa.
19
Kwa hekima Bwana aliiweka misingi ya dunia, kwa ufahamu aliziweka mbingu mahali pake;
20
kwa maarifa yake vilindi viligawanywa, nayo mawingu yanadondosha umande.

Hekima Hutoa Usalama na Amani

21
Mwanangu, hifadhi maamuzi mema na busara, usiache vitoke machoni pako;
22
ndipo vitakapokuwa uzima nafsini mwako na pambo la neema shingoni mwako.
23
Kisha utaenda katika njia yako salama, wala mguu wako hautajikwaa;
24
ulalapo, hautaogopa; ulalapo usingizi wako utakuwa mtamu.
25
Usiogope maafa ya ghafula au maangamizi yanayowapata waovu,
26
kwa kuwa Bwana atakuwa tumaini lako na kuepusha mguu wako kunaswa katika mtego.

Ishi kwa Haki na Jirani Zako

27
Usizuie wema kwa wale wanaostahili ikiwa katika uwezo wako kutenda.
28
Usimwambie jirani yako, “Njoo baadaye, nitakupa kesho”: wakati wewe unacho kitu kile karibu nawe.
29
Usifanye hila ya kumdhuru jirani yako, ambaye anaishi karibu na wewe akikuamini.
30
Usimshtaki mtu bila sababu, wakati hajakutenda dhara lolote.
31
Usimwonee wivu mtu mwenye jeuri wala kuchagua njia yake iwayo yote,
32
kwa kuwa Bwana humchukia mtu mpotovu, lakini siri yake iko kwa mwenye haki.
33
Laana ya Bwana i juu ya nyumba ya mwovu, lakini yeye huibariki nyumba ya mwenye haki.
34
Huwadhihaki wale wanaodhihaki, lakini huwapa neema wale wanyenyekevu.
35
Wenye hekima hurithi heshima, bali huwaaibisha wapumbavu.
Use arrow keys to navigate
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Reading Width 45 chars

Options