Skip to content

1 Wakorintho4

Watumishi na Wasimamizi wa Mungu

1
Basi, watu na watuhesabu sisi kuwa tu watumishi wa Kristo na mawakili wa siri za Mungu.
2
Tena, litakiwalo ni mawakili waonekane kuwa waaminifu.
3
Lakini kwangu mimi ni jambo dogo sana kwamba nihukumiwe na ninyi au na mahakama yoyote ya kibinadamu. Naam, hata mimi mwenyewe sijihukumu.
4
Dhamiri yangu ni safi, lakini hilo halinihesabii kuwa asiye na hatia. Bwana ndiye anihukumuye.
5
Kwa hiyo msihukumu jambo lolote kabla ya wakati wake. Ngojeni mpaka Bwana atakapokuja. Yeye atayaleta nuruni mambo yale yaliyofichwa gizani, na kuweka wazi nia za mioyo ya wanadamu. Wakati huo kila mmoja atapokea sifa anayostahili kutoka kwa Mungu.

Onyo Dhidi ya Kiburi na Kujisifu

6
Basi ndugu zangu, mambo haya nimeyafanya kwangu binafsi na Apolo kwa faida yenu, ili mweze kujifunza kutoka kwetu maana ya ule usemi usemao, “Msivuke zaidi ya yale yaliyoandikwa.” Hivyo hamtajivunia mtu fulani na kumdharau mwingine.
7
Kwa maana ni nani aliyewafanya kuwa tofauti na wengine? Ni nini mlicho nacho ambacho hamkupokea? Nanyi kama mlipokea, kwa nini mnajivuna kama vile hamkupokea?

Mateso ya Mitume

8
Sasa tayari mnayo yale yote mnayohitaji! Tayari mmekwisha kuwa matajiri! Mmekuwa wafalme, tena bila sisi! Laiti mngekuwa wafalme kweli ili na sisi tupate kuwa wafalme pamoja nanyi!
9
Kwa maana ninaona kwamba Mungu ametuweka sisi mitume katika nafasi ya mwisho kabisa, kama watu waliohukumiwa kufa kwenye uwanja wa tamasha, kwa sababu tumefanywa kuwa maonyesho kwa ulimwengu wote, kwa malaika na kwa wanadamu pia.
10
Kwa ajili ya Kristo sisi ni wajinga, lakini ninyi mna hekima sana ndani ya Kristo. Sisi tu dhaifu, lakini ninyi mna nguvu. Tunadharauliwa, lakini ninyi mnaheshimiwa.
11
Mpaka saa hii tuna njaa na kiu, tu uchi, tumepigwa na hatuna makao.
12
Tunafanya kazi kwa bidii kwa mikono yetu wenyewe. Tunapolaaniwa, tunabariki, tunapoteswa, tunastahimili,
13
tunaposingiziwa, tunajibu kwa upole. Mpaka sasa tumekuwa kama takataka ya dunia na uchafu wa ulimwengu.

Onyo la Paulo la Kibaba

14
Siwaandikii mambo haya ili kuwaaibisha, bali ili kuwaonya, kama wanangu wapendwa.
15
Hata kama mnao walimu 10,000 katika Kristo, lakini hamna baba wengi. Mimi nilikuwa baba yenu katika Kristo Yesu kwa kuwaletea Injili.
16
Basi nawasihi igeni mfano wangu.
17
Kwa sababu hii ninamtuma Timotheo, mwanangu mpendwa na mwaminifu katika Bwana. Yeye atawakumbusha kuhusu njia za maisha yangu katika Kristo Yesu, ambayo yanakubaliana na mafundisho yangu ninayofundisha katika kila kanisa.

Jaribio la Nguvu

18
Baadhi yenu mmekuwa na jeuri mkidhani kuwa sitafika kwenu.
19
Lakini kama Bwana akipenda, nitafika kwenu mapema, nami nitapenda kujua, si tu kile wanachosema hawa watu jeuri, bali pia kujua nguvu yao.
20
Kwa kuwa Ufalme wa Mungu si maneno matupu tu bali ni nguvu.
21
Ninyi amueni. Je, nije kwenu na fimbo, au nije kwa upendo na kwa roho ya upole?
Use arrow keys to navigate
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Reading Width 45 chars

Options