Hesabu 10:1-16
1
Bwana akamwambia Mose:
2
“Tengeneza tarumbeta mbili za fedha ya kufua, uzitumie kwa kuita jumuiya pamoja na wakati wa kuvunja makambi ili kuondoka.
3
Tarumbeta zote mbili zikipigwa, jumuiya yote itakusanyika mbele yako katika ingilio la Hema la Kukutania.
4
Kama tarumbeta moja tu ikipigwa, viongozi, yaani wakuu wa koo za Israeli, ndio watakaokusanyika mbele yako.
5
Wakati mlio wa kujulisha hatari ukipigwa, makabila yaliyo na makambi upande wa mashariki yataondoka.
6
Ukisikika mlio wa pili wa jinsi hiyo, walioko kwenye makambi ya kusini wataondoka. Mlio huo wa kujulisha hatari utakuwa ishara ya kuondoka.
7
Ili kukusanya kusanyiko, piga tarumbeta zote, lakini siyo kwa mlio wa kujulisha hatari.
8
“Wana wa Aroni, makuhani, ndio watakaopiga hizo tarumbeta. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa ajili yenu na kwa vizazi vijavyo.
9
Wakati mtakapopigana vita katika nchi yenu wenyewe dhidi ya adui anayewaonea, piga tarumbeta kwa mlio wa kujulisha hatari. Ndipo utakumbukwa na Bwana Mungu wenu na kuokolewa kutoka kwa adui zenu.
10
Pia nyakati za furaha yenu, yaani sikukuu zenu zilizoamriwa na sikukuu za Mwezi Mwandamo, mtapiga tarumbeta juu ya sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka zenu za amani, nazo zitakuwa ukumbusho kwa ajili yenu mbele za Mungu wenu. Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.”
11
Katika siku ya ishirini ya mwezi wa pili wa mwaka wa pili, wingu liliinuka kutoka juu ya maskani ya Ushuhuda.
12
Ndipo Waisraeli wakaondoka kutoka Jangwa la Sinai wakasafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine mpaka wingu lilipotua katika Jangwa la Parani.
13
Waliondoka kwa mara ya kwanza kwa agizo la Bwana kupitia kwa Mose.
14
Vikosi vya kambi ya Yuda vilitangulia kwanza chini ya alama yao. Nashoni mwana wa Aminadabu alikuwa kiongozi wao.
15
Nethaneli mwana wa Suari alikuwa kiongozi wa kabila la Isakari,
16
naye Eliabu mwana wa Heloni alikuwa kiongozi wa kabila la Zabuloni.
Maandiko ya Biblia: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu)™, © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. · CC BY-SA 4.0“Biblica” is a trademark registered in the United States Patent and Trademark Office by Biblica, Inc., used with permission.
Settings