Mathayo 8:1-17
1
Yesu aliposhuka kutoka mlimani, makutano makubwa ya watu yakamfuata.
2
Mtu mmoja mwenye ukoma akaja na kupiga magoti mbele yake, akasema, “Bwana, kama ukitaka, unaweza kunitakasa.”
3
Yesu akanyoosha mkono wake akamgusa yule mtu, akamwambia, “Nataka. Takasika!” Mara yule mtu akatakasika ukoma wake.
4
Kisha Yesu akamwambia, “Hakikisha humwambii mtu yeyote. Lakini nenda ukajionyeshe kwa kuhani, na utoe sadaka aliyoamuru Mose, ili kuwa ushuhuda kwao.”
5
Yesu alipoingia Kapernaumu, jemadari mmoja alimjia, kumwomba msaada,
6
akisema, “Bwana, mtumishi wangu amelala nyumbani na amepooza, tena ana maumivu makali ya kutisha.”
7
Yesu akamwambia, “Nitakuja na kumponya.”
8
Lakini yule jemadari akamwambia, “Bwana, mimi sistahili wewe kuingia chini ya dari yangu. Lakini sema neno tu, naye mtumishi wangu atapona.
9
Kwa kuwa mimi mwenyewe ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, nikiwa na askari chini yangu. Nikimwambia huyu, ‘Nenda,’ yeye huenda; na mwingine nikimwambia, ‘Njoo,’ yeye huja. Nikimwambia mtumishi wangu, ‘Fanya hivi,’ yeye hufanya.”
10
Yesu aliposikia maneno haya, alishangaa, akawaambia wale waliomfuata, “Amin, nawaambia, hata katika Israeli sijapata kuona yeyote mwenye imani kubwa namna hii.
11
Ninawaambia kwamba wengi watatoka mashariki na magharibi, nao wataketi karamuni pamoja na Abrahamu, Isaki na Yakobo katika Ufalme wa Mbinguni.
12
Lakini warithi wa Ufalme watatupwa katika giza la nje, ambako kutakuwako kilio na kusaga meno.”
13
Kisha Yesu akamwambia yule jemadari, “Nenda na iwe kwako sawasawa na imani yako.” Naye yule mtumishi akapona saa ile ile.
14
Yesu alipoingia nyumbani kwa Petro, alimkuta mama mkwe wa Petro amelala kitandani, akiwa ana homa.
15
Akamgusa mkono wake na homa ikamwacha, naye akainuka na kuanza kumhudumia.
16
Jioni ile, wakamletea watu wengi waliopagawa na pepo wachafu, naye akawatoa wale pepo wachafu kwa neno lake, na kuwaponya wagonjwa wote.
17
Haya yalifanyika ili litimie lile lililonenwa kwa kinywa cha nabii Isaya kwamba: “Mwenyewe alitwaa udhaifu wetu na alichukua magonjwa yetu.”
Settings