Marko 9:32-50
32
Lakini wao hawakuelewa kile alimaanisha, nao waliogopa kumuuliza maana yake.
33
Basi wakafika Kapernaumu na baada ya kuingia nyumbani akawauliza, “Mlikuwa mnabishana nini kule njiani?”
34
Lakini hawakumjibu, kwa sababu njiani walikuwa wakibishana kuhusu nani miongoni mwao alikuwa mkuu zaidi ya wote.
35
Akaketi chini, akawaita wote kumi na wawili, akawaambia: “Kama mtu yeyote akitaka kuwa wa kwanza, hana budi kuwa wa mwisho na mtumishi wa wote.”
36
Kisha akamchukua mtoto mdogo, akamsimamisha katikati yao. Akamkumbatia, akawaambia,
37
“Mtu yeyote amkaribishaye mmoja wa hawa watoto wadogo kwa Jina langu, anikaribisha mimi. Naye anikaribishaye mimi, amkaribisha Baba yangu aliyenituma.”
38
Yohana akamwambia, “Mwalimu, tumemwona mtu akitoa pepo wachafu kwa jina lako, nasi tukamkataza, kwa sababu yeye si mmoja wetu.”
39
Yesu akasema, “Msimkataze, kwa kuwa hakuna yeyote atendaye miujiza kwa Jina langu ambaye baada ya kitambo kidogo aweza kunena lolote baya dhidi yangu.
40
Kwa maana yeyote asiye kinyume chetu, yuko upande wetu.
41
Amin, nawaambia, yeyote awapaye ninyi kikombe cha maji kwa Jina langu kwa sababu ninyi ni mali ya Kristo, hakika hataikosa thawabu yake.”
42
“Kama mtu yeyote akimsababisha mmojawapo wa wadogo hawa wanaoniamini kutenda dhambi, ingekuwa bora kwake afungiwe jiwe kubwa la kusagia shingoni mwake, na kutoswa baharini.
43
Kama mkono wako ukikusababisha kutenda dhambi, ukate. Ni afadhali kwako kuingia katika uzima ukiwa na mkono mmoja, kuliko kuwa na mikono miwili lakini ukaingia jehanamu, mahali ambako moto hauzimiki. [
44
Mahali ambako funza wake hawafi wala moto wake hauzimiki.]
45
Kama mguu wako ukikusababisha kutenda dhambi, ukate. Ni afadhali kwako kuingia katika uzima ukiwa kiwete, kuliko kuwa na miguu miwili lakini ukaingia jehanamu. [
46
Mahali ambako funza wake hawafi wala moto hauzimiki.]
47
Nalo jicho lako likikusababisha kutenda dhambi, lingʼoe. Ni afadhali kwako kuingia katika Ufalme wa Mungu ukiwa na jicho moja, kuliko kuwa na macho mawili lakini ukatupwa jehanamu,
48
mahali ambako “ ‘funza wake hawafi, wala moto wake hauzimiki.’
49
Kila mmoja atatiwa chumvi kwa moto.
50
“Chumvi ni nzuri, lakini ikipoteza ladha yake utaifanyaje ili iweze kukolea tena? Mwe na chumvi ndani yenu, mkaishi kwa amani, kila mmoja na mwenzake.”
Settings