Yohana 6:13-37
13
Hivyo wakavikusanya, wakajaza vikapu kumi na viwili kwa vipande vya ile mikate mitano ya shayiri na samaki wale wawili wadogo vilivyobakishwa na waliokula.
14
Baada ya watu kuona muujiza ule Yesu aliofanya, walianza kusema, “Hakika huyu ndiye Nabii ajaye ulimwenguni!”
15
Yesu akijua kwamba walitaka kuja kumfanya awe mfalme wao, kwa nguvu, akajitenga nao akaenda milimani peke yake.
16
Ilipofika jioni, wanafunzi wake waliteremka kwenda baharini.
17
Wakaingia kwenye mashua, wakaanza kuvuka bahari kwenda Kapernaumu. Wakati huu kulikuwa tayari giza na Yesu alikuwa hajajumuika nao.
18
Bahari ikachafuka kwa sababu upepo mkali ulikuwa unavuma.
19
Wanafunzi walipokuwa wamekwenda mwendo wa karibu maili tatu au nne, walimwona Yesu akitembea juu ya maji akikaribia mashua, nao wakaogopa sana.
20
Lakini Yesu akawaambia, “Ni mimi. Msiogope.”
21
Ndipo wakamkaribisha kwa furaha ndani ya mashua, na mara wakafika ufuoni walikokuwa wakienda.
22
Siku iliyofuata, wale watu waliokuwa wamebaki ngʼambo waliona kwamba palikuwepo na mashua moja tu na kwamba Yesu hakuwa ameondoka pamoja na wanafunzi wake, ila walikuwa wameondoka peke yao.
23
Lakini zikaja mashua nyingine kutoka Tiberia zikafika karibu na mahali pale walipokula mikate baada ya Bwana kumshukuru Mungu.
24
Mara wale watu wakatambua kwamba Yesu hakuwepo hapo, wala wanafunzi wake. Wakaingia kwenye mashua hizo, wakaenda Kapernaumu ili kumtafuta Yesu.
25
Walipomkuta Yesu ngʼambo ya bahari wakamuuliza, “Rabi, umefika lini huku?”
26
Yesu akawajibu, “Amin, amin nawaambia, ninyi hamnitafuti kwa kuwa mliona ishara na miujiza, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba.
27
Msishughulikie chakula kiharibikacho, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele, ambacho Mwana wa Adamu atawapa. Yeye ndiye ambaye Mungu Baba amemtia muhuri.”
28
Ndipo wakamuuliza, “Tufanye nini ili tupate kuitenda kazi ya Mungu?”
29
Yesu akawajibu, “Kazi ya Mungu ndiyo hii: Mwaminini yeye aliyetumwa naye.”
30
Hivyo wakamuuliza, “Utafanya ishara gani ya muujiza, ili tuione tukuamini? Utafanya jambo gani?
31
Baba zetu walikula mana jangwani, kama ilivyoandikwa, ‘Aliwapa mikate kutoka mbinguni ili wale.’ ”
32
Yesu akawaambia, “Amin, amin nawaambia, si Mose aliyewapa mikate kutoka mbinguni, bali Baba yangu ndiye anawapa mkate wa kweli kutoka mbinguni.
33
Kwa maana mkate wa Mungu ni yule ashukaye kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima.”
34
Wakamwambia, “Bwana, kuanzia sasa tupatie huo mkate siku zote.”
35
Yesu akawaambia, “Mimi ndimi mkate wa uzima. Yeye ajaye kwangu, hataona njaa kamwe na yeye aniaminiye, hataona kiu kamwe.
36
Lakini kama nilivyowaambia, mmeniona lakini bado hamwamini.
37
Wale wote anipao Baba watakuja kwangu na yeyote ajaye kwangu, sitamfukuzia nje kamwe.
Settings