Yohana 4:39-54
39
Wasamaria wengi katika mji ule wakamwamini Yesu kwa sababu ya ushuhuda wa yule mwanamke alipowaambia kwamba, “Ameniambia kila kitu nilichotenda.”
40
Hivyo wale Wasamaria walipomjia, wakamsihi akae kwao. Naye akakaa huko siku mbili.
41
Kwa sababu ya neno lake, watu wengi wakaamini.
42
Wakamwambia yule mwanamke, “Sasa tunaamini, wala si kwa sababu ya maneno yako tu, bali kwa kuwa tumemsikia sisi wenyewe. Tumejua hakika kweli ya kwamba huyu ndiye Kristo, Mwokozi wa ulimwengu.”
43
Baada ya zile siku mbili, Yesu aliondoka kwenda Galilaya.
44
(Basi Yesu mwenyewe alikuwa amesema kwamba nabii hapati heshima katika nchi yake mwenyewe.)
45
Alipofika Galilaya, Wagalilaya walimkaribisha, kwani walikuwa wameona yale aliyoyatenda huko Yerusalemu wakati wa Sikukuu ya Pasaka. Kwa maana wao pia walikuwa wamehudhuria hiyo Sikukuu.
46
Hivyo Yesu akaja tena mpaka Kana ya Galilaya, kule alikokuwa amebadili maji kuwa divai. Huko kulikuwepo na afisa mmoja wa mfalme, ambaye mwanawe alikuwa mgonjwa huko Kapernaumu.
47
Huyo mtu aliposikia kwamba Yesu alikuwa amewasili Galilaya kutoka Uyahudi, alimwendea na kumwomba ili aje kumponya mwanawe, aliyekuwa mgonjwa karibu ya kufa.
48
Yesu akamwambia, “Ninyi watu msipoona ishara na miujiza kamwe hamtaamini.”
49
Yule afisa wa mfalme akamwambia, “Bwana, tafadhali shuka kabla mwanangu hajafa.”
50
Yesu akamjibu, “Enenda zako, mwanao yu hai.” Yule afisa akaamini yale maneno Yesu aliyomwambia, akaondoka akaenda zake.
51
Alipokuwa bado yuko njiani, akakutana na watumishi wake wakamwambia kwamba mwanawe yu mzima.
52
Akawauliza saa ambayo alianza kupata nafuu. Wakamwambia, “Jana yapata saa saba, homa ilimwacha.”
53
Ndipo baba wa huyo mtoto akakumbuka kuwa huo ndio wakati ambapo Yesu alikuwa amemwambia, “Mwanao yu hai.” Kwa hiyo yeye pamoja na wote wa nyumbani mwake wakamwamini Yesu.
54
Hii ilikuwa ishara ya pili ambayo Yesu alifanya aliporudi Galilaya kutoka Uyahudi.
Settings