Skip to content
Yohana 12:20-36

Yohana 12:20-36

20
Basi palikuwa Wayunani fulani miongoni mwa wale waliokuwa wamekwenda kuabudu wakati wa Sikukuu.
21
Hawa wakamjia Filipo, ambaye alikuwa mwenyeji wa Bethsaida huko Galilaya, wakiwa na ombi. Wakamwambia, “Tungependa kumwona Yesu.”
22
Filipo akaenda akamweleza Andrea, nao wote wawili wakamwambia Yesu.
23
Yesu akawajibu, “Saa imewadia ya Mwana wa Adamu kutukuzwa.
24
Amin, amin nawaambia, mbegu ya ngano isipoanguka ardhini na kufa, hubakia kama mbegu peke yake. Lakini ikifa huzaa mbegu nyingi.
25
Mtu yeyote anayependa maisha yake atayapoteza, naye ayachukiaye maisha yake katika ulimwengu huu atayaokoa hata kwa uzima wa milele.
26
Mtu yeyote akinitumikia lazima anifuate, nami mahali nilipo ndipo mtumishi wangu atakapokuwa. Mtu akinitumikia, Baba yangu atamheshimu.
27
“Sasa roho yangu imefadhaika sana. Niseme nini? ‘Baba, niokoe katika saa hii.’ Lakini ni kwa kusudi hili nimeufikia wakati huu.
28
Baba, litukuze jina lako.” Ndipo ikaja sauti kutoka mbinguni, “Nimelitukuza, nami nitalitukuza tena.”
29
Ule umati wa watu uliokuwa mahali pale uliisikia nao ukasema, “Hiyo ni sauti ya radi,” wengine wakasema, “Malaika ameongea naye.”
30
Yesu akawaambia, “Sauti hii imesikika kwa faida yenu, wala si kwa faida yangu.
31
Sasa ni saa ya hukumu kwa ajili ya ulimwengu huu, sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje.
32
Lakini mimi, nikiinuliwa kutoka nchi, nitawavuta watu wote waje kwangu.”
33
Yesu aliyasema haya akionyesha ni kifo gani atakachokufa.
34
Ule umati wa watu ukapiga kelele ukasema, “Tumesikia kutoka Sheria kwamba ‘Kristo adumu milele,’ wewe wawezaje kusema, ‘Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa juu’? Huyu ‘Mwana wa Adamu’ ni nani?”
35
Ndipo Yesu akawaambia, “Bado kitambo kidogo nuru ingalipo pamoja nanyi. Enendeni maadamu mna nuru, msije mkakumbwa na giza. Mtu anayetembea gizani hajui anakokwenda.
36
Wekeni tumaini lenu katika nuru hiyo ili mpate kuwa wana wa nuru.” Baada ya kusema haya, Yesu aliondoka, akajificha wasimwone.
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Options