Ayubu 15:17-35
17
“Nisikilize mimi nami nitakueleza, acha nikuambie yale niliyoyaona,
18
ambayo watu wenye hekima wameyanena, bila kuficha lolote walilopokea toka kwa baba zao
19
(wakati ambao wao peke yao ndio walipewa nchi, hakuna mgeni aliyepita miongoni mwao):
20
Mtu mwovu siku zake zote hupata mateso, miaka yote aliwekewa mkorofi.
21
Sauti za kutisha hujaa masikioni mwake; katika kufanikiwa kwake, wanyangʼanyi humshambulia.
22
Hukata tamaa kuokoka gizani; amewekwa kwa ajili ya upanga.
23
Hutangatanga, akitafuta chakula; anajua kwamba siku ya giza iko karibu.
24
Taabu na maumivu makuu vinamtia hofu; humshinda kama mfalme aliye tayari kwa vita,
25
kwa sababu amemkunjia Mungu ngumi yake na kujigamba dhidi ya Mwenyezi,
26
kwa kiburi akishambulia dhidi ya Mungu akiwa na ngao nene, iliyo imara.
27
“Ingawa uso wake umefunikwa na mafuta kwa unene na kiuno chake kimevimba kwa kunenepa,
28
ataishi katika miji ya magofu, na katika nyumba ambazo haziishi mwanadamu yeyote, nyumba zinazokuwa vifusi.
29
Hatatajirika tena, nao utajiri wake hautadumu, wala mali zake hazitakuwa nyingi juu ya nchi.
30
Hatatoka gizani; mwali wa moto utanyausha machipukizi yake, nayo pumzi ya kinywa cha Mungu itamwondolea mbali.
31
Asijidanganye mwenyewe kutumainia ubatili, kwa kuwa hatapata malipo yoyote.
32
Atakuwa amelipwa kikamilifu kabla ya wakati wake, nayo matawi yake hayatastawi.
33
Atafanana na mzabibu uliopukutishwa matunda yake kabla hayajaiva, kama mzeituni unaodondosha maua yake.
34
Kwa kuwa jamii ya wasiomcha Mungu watakuwa tasa, nao moto utateketeza hema za wale wanaopenda rushwa.
35
Hutunga mimba ya madhara na kuzaa uovu; matumbo yao huumba udanganyifu.”
Settings