Yeremia 6:16-30
16
Hivi ndivyo asemavyo Bwana: “Simama kwenye njia panda utazame, ulizia mapito ya zamani, ulizia wapi ilipo njia nzuri, uifuate hiyo, nanyi mtapata raha nafsini mwenu. Lakini ninyi mlisema, ‘Hatutaipita hiyo.’
17
Niliweka walinzi juu yenu na kusema, ‘Sikieni sauti ya tarumbeta!’ Lakini mkasema, ‘Hatutasikiliza.’
18
Kwa hiyo sikilizeni, enyi mataifa, angalieni, enyi mashahidi, lile litakalowatokea.
19
Sikia, ee nchi: Ninaleta maafa juu ya watu hawa, matunda ya mipango yao, kwa sababu hawakusikiliza maneno yangu na wameikataa sheria yangu.
20
Unanifaa nini uvumba kutoka Sheba, au udi wa harufu nzuri kutoka nchi ya mbali? Sadaka zako za kuteketezwa hazikubaliki, dhabihu zako hazinifurahishi mimi.”
21
Kwa hiyo hivi ndivyo asemavyo Bwana: “Nitaweka vikwazo mbele ya watu hawa. Baba na wana wao watajikwaa juu yake, majirani na marafiki wataangamia.”
22
Hivi ndivyo asemavyo Bwana: “Tazama, jeshi linakuja kutoka nchi ya kaskazini, taifa kubwa linaamshwa kutoka miisho ya dunia.
23
Wamejifunga pinde na mkuki, ni wakatili na hawana huruma. Wanatoa sauti kama bahari inayonguruma wanapoendesha farasi zao. Wanakuja kama watu waliojipanga tayari kwa vita ili kukushambulia, ee Binti Sayuni.”
24
Tumesikia taarifa zao, nayo mikono yetu imelegea. Uchungu umetushika, maumivu kama ya mwanamke katika utungu wa kuzaa.
25
Usitoke kwenda mashambani au kutembea barabarani, kwa kuwa adui ana upanga, na kuna vitisho kila upande.
26
Enyi watu wangu, vaeni magunia mjivingirishe kwenye majivu, ombolezeni kwa kilio cha uchungu kama amliliaye mwana pekee, kwa maana ghafula mharabu atatujia.
27
“Nimekufanya wewe kuwa kitu cha kujaribu chuma, nao watu wangu kama mawe yenye madini, ili upate kuzijua na kuzijaribu njia zao.
28
Wote ni waasi sugu, wakienda huku na huko kusengenya. Wao ni shaba na chuma, wote wanatenda upotovu.
29
Mivuo inavuma kwa nguvu, kinachoungua kwa huo moto ni risasi, lakini pamoja na kusafisha kote huku ni bure; waovu hawaondolewi.
30
Wanaitwa fedha iliyokataliwa, kwa sababu Bwana amewakataa.”
Maandiko ya Biblia: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu)™, © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. · CC BY-SA 4.0“Biblica” is a trademark registered in the United States Patent and Trademark Office by Biblica, Inc., used with permission.
Settings