Skip to content
Isaya 44:6-20

Isaya 44:6-20

6
“Hili ndilo asemalo Bwana, Mfalme wa Israeli na Mkombozi, Bwana Mwenye Nguvu Zote: Mimi ni wa kwanza na Mimi ni wa mwisho; zaidi yangu hakuna Mungu.
7
Ni nani basi aliye kama mimi? Yeye na atangaze. Yeye atangaze na kuweka mbele yangu ni kitu gani kilichotokea tangu nilipoumba watu wangu wa kale, tena ni nini kitakachotokea: naam, yeye na atoe unabii ni nini kitakachokuja.
8
Msitetemeke, msiogope. Je, sikutangaza hili, na kutoa unabii tangu zamani? Ninyi ni mashahidi wangu. Je, yuko Mungu zaidi yangu mimi? Hasha, hakuna Mwamba mwingine; mimi simjui mwingine.”
9
Wote wachongao sanamu ni ubatili, navyo vitu wanavyovithamini havifai kitu. Wale ambao wanazitetea ni vipofu, ni wajinga, nao waaibika.
10
Ni nani atengenezaye mungu na kusubu sanamu, ambayo haiwezi kumfaidia kitu chochote?
11
Yeye pamoja na wenziwe wa aina yake wataaibishwa, mafundi wao si kitu ila ni wanadamu tu. Wote wakusanyike pamoja na kuwa na msimamo wao, watashushwa chini kwa hofu na kwa fedheha.
12
Muhunzi huchukua kifaa na kukifanyia kazi kwenye makaa ya moto, hutengeneza sanamu kwa nyundo, huifanyiza kwa nguvu za mkono wake. Huona njaa na kupoteza nguvu zake, asipokunywa maji huzimia.
13
Seremala hupima kwa kutumia kamba na huuchora mstari kwa kalamu; huchonga kwa patasi na kutia alama kwa bikari. Huifanyiza katika umbo la binadamu, la mwanadamu katika utukufu wake wote, ili iweze kukaa katika sehemu yake ya ibada ya miungu.
14
Hukata miti ya mierezi, huchukua mtiriza au mwaloni. Huuacha ukue miongoni mwa miti ya msituni, au hupanda msunobari, nayo mvua huufanya ukue.
15
Ni kuni ya binadamu: yeye huchukua baadhi yake na kuota moto, huwasha moto na kuoka mkate. Lakini pia huutumia kumtengeneza mungu na akamwabudu, huitengeneza sanamu na kuisujudia.
16
Sehemu ya kuni huziweka motoni, akapikia chakula chake, hubanika nyama na kula hadi ashibe. Huota moto na kusema, “Aha! Ninahisi joto, ninaona moto.”
17
Mabaki yake hutengeneza mungu, sanamu yake; yeye huisujudia na kuiabudu. Huiomba na kusema, “Niokoe; wewe ni mungu wangu.”
18
Hawajui chochote, hawaelewi chochote, macho yao yamefungwa hata hawawezi kuona, akili zao zimefungwa hata hawawezi kufahamu.
19
Hakuna anayefikiri, hakuna mwenye maarifa wala ufahamu wa kusema, “Sehemu yake nilitumia kwa kuni; hata pia nilioka mkate juu ya makaa yake, nikabanika nyama na kuila. Je, nifanye machukizo kwa kile kilichobaki? Je, nisujudie gogo la mti?”
20
Hujilisha kwa majivu, moyo uliodanganyika humpotosha; hawezi kujiokoa mwenyewe, au kusema, “Je, kitu hiki kilichoko katika mkono wangu wa kuume si ni uongo?”
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Options