Skip to content
Mwanzo 32:15-32

Mwanzo 32:15-32

15
Ngamia wake thelathini pamoja na ndama zao, ngʼombe wake arobaini na mafahali kumi, punda wake ishirini na punda waume kumi.
16
Akaviweka chini ya uangalizi wa watumishi wake, kila kundi peke yake na kuwaambia, “Nitangulieni na kuacha nafasi kati ya makundi.”
17
Akamwagiza yule aliyetangulia kuwa, “Ndugu yangu Esau atakapokutana nawe na kukuuliza, ‘Wewe ni wa nani? Unakwenda wapi? Wanyama hawa wote mbele yako ni mali ya nani?’
18
Ndipo utakaposema, ‘Ni mali ya mtumishi wako Yakobo. Ni zawadi ambazo zimetumwa kwa bwana wangu Esau, naye anakuja nyuma yetu.’ ”
19
Akamwagiza pia yule mtumishi wa kundi la pili, la tatu na yale mengine yote yaliyofuata akiwaambia, “Mtamwambia Esau maneno hayo hayo mtakapokutana naye.
20
Hakikisheni mmesema, ‘Mtumishi wako Yakobo anakuja nyuma yetu.’ ” Kwa kuwa alifikiri, “Nitaweza kumtuliza kwa zawadi hizi ninazotanguliza, hatimaye, nitakapomwona, huenda atanikubali.”
21
Kwa hiyo zawadi za Yakobo zilitangulia mbele yake, lakini yeye mwenyewe alilala kambini usiku ule.
22
Usiku ule Yakobo akaamka akawachukua wake zake wawili, watumishi wake wawili wa kike na wanawe kumi na mmoja na akavuka kivuko cha Yaboki.
23
Baada ya kuwavusha ngʼambo ya kijito, alivusha pia mali zake zote.
24
Kwa hiyo Yakobo akaachwa peke yake na mtu mmoja akashikana naye mweleka mpaka mapambazuko.
25
Yule mtu alipoona kuwa hawezi kumshinda, aligusa kiungio cha nyonga ya Yakobo kwa hiyo nyonga yake ikateguka wakati alipokuwa akishikana mweleka na yule mtu.
26
Ndipo yule mtu akasema, “Niache niende, kwa kuwa ni mapambazuko.” Lakini Yakobo akajibu, “Sitakuacha uende usiponibariki.”
27
Yule mtu akamuuliza, “Jina lako nani?” Akajibu, “Yakobo.”
28
Ndipo yule mtu akasema, “Jina lako halitakuwa tena Yakobo, bali Israeli, kwa sababu umeshindana na Mungu na watu pia, nawe umeshinda.”
29
Yakobo akasema, “Tafadhali niambie jina lako.” Lakini akajibu, “Kwa nini kuniuliza Jina langu?” Ndipo akambariki huko.
30
Kwa hiyo Yakobo akapaita mahali pale Penieli, akasema, “Ni kwa sababu nimemwona Mungu uso kwa uso na bado maisha yangu yameokoka.”
31
Jua lilikuwa linachomoza Yakobo alipoondoka Penueli, naye alikuwa akichechemea kwa sababu ya nyonga yake.
32
Kwa hiyo mpaka leo Waisraeli hawali mshipa ulioungana na kiungio cha nyonga, kwa sababu kiungio cha nyonga ya Yakobo kiliteguliwa karibu na mshipa huo.

Maandiko ya Biblia: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu)™, © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. · CC BY-SA 4.0“Biblica” is a trademark registered in the United States Patent and Trademark Office by Biblica, Inc., used with permission.

Settings

Reading style

Typeface

Font size 19px

Reading width 75 chars

Options