Skip to content
Kutoka 23:1-19

Kutoka 23:1-19

1
“Usieneze habari za uongo. Usimsaidie mtu mwovu kwa kuwa shahidi mwenye nia ya kudhuru wengine.
2
“Usifuate umati wa watu katika kutenda mabaya. Unapotoa ushahidi kwenye mashtaka, usipotoshe haki ukijumuika na umati wa watu,
3
nawe usimpendelee mtu maskini katika mashtaka yake.
4
“Kama ukikutana na maksai au punda wa adui yako anapotea, hakikisha umemrudisha kwake.
5
Ukiona punda wa mtu anayekuchukia ameanguka na mzigo wake, usimwache hapo alipoangukia; hakikisha kuwa umemsaidia.
6
“Usiwanyime haki watu wako walio maskini katika mashtaka yao.
7
Ujiepushe na mashtaka ya uongo, wala usimuue mtu asiye na hatia au mtu mwaminifu, kwa maana sitamhesabia hana hatia yeye aliye na hatia.
8
“Usipokee rushwa, kwa kuwa rushwa hupofusha wale waonao, na kupinda maneno ya wenye haki.
9
“Usimwonee mgeni; ninyi wenyewe mnajua jinsi mgeni anavyojisikia, kwa sababu mlikuwa wageni Misri.
10
“Kwa muda wa miaka sita mtapanda mashamba yenu na kuvuna mazao,
11
lakini katika mwaka wa saba usiilime ardhi wala kuitumia, ili watu walio maskini miongoni mwenu waweze kupata chakula kutoka kwenye hayo mashamba, nao wanyama pori wapate chakula kwa yale mabaki watakayobakiza. Utafanya hivyo katika shamba lako la mizabibu na la mizeituni.
12
“Kwa siku sita fanya kazi zako, lakini siku ya saba usifanye kazi, ili maksai wako na punda wako wapate kupumzika, naye mtumwa aliyezaliwa nyumbani mwako, pamoja na mgeni, wapate kustarehe.
13
“Uzingatie kutenda kila kitu nilichokuambia. Usiombe kwa majina ya miungu mingine, wala usiyaruhusu kusikika kinywani mwako.
14
“Mara tatu kwa mwaka utanifanyia sikukuu.
15
“Utaadhimisha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu; kwa siku saba utakula mikate isiyotiwa chachu kama nilivyokuagiza. Fanya jambo hili kwa wakati uliopangwa katika mwezi wa Abibu, ndio mwezi wa nne, kwa sababu katika mwezi huo ulitoka Misri. “Mtu yeyote asije mbele yangu mikono mitupu.
16
“Utaadhimisha Sikukuu ya Mavuno kwa malimbuko ya mazao yako uliyopanda katika shamba lako. “Utaadhimisha Sikukuu ya Kukusanya mavuno mwishoni mwa mwaka, unapokusanya mavuno yako toka shambani.
17
“Mara tatu kwa mwaka wanaume wote watakuja mbele za Bwana Mwenyezi.
18
“Msitoe damu ya dhabihu kwangu pamoja na kitu chochote kilicho na chachu. “Mafuta ya mnyama wa sadaka ya sikukuu yangu yasibakizwe mpaka asubuhi.
19
“Utaleta malimbuko bora ya ardhi yako katika nyumba ya Bwana Mungu wako. “Usimchemshe mwana-mbuzi katika maziwa ya mama yake.
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Options