Kutoka 15:13-27
13
“Katika upendo wako usiokoma utawaongoza watu uliowakomboa. Katika nguvu zako utawaongoza mpaka makao yako matakatifu.
14
Mataifa watasikia na kutetemeka, uchungu utawakamata watu wa Ufilisti.
15
Wakuu wa Edomu wataogopa, viongozi wa Moabu watatetemeka kwa hofu, watu wa Kanaani watayeyuka,
16
vitisho na hofu vitawaangukia. Kwa nguvu ya mkono wako watatulia kama jiwe, mpaka watu wako waishe kupita, Ee Bwana, mpaka watu uliowanunua wapite.
17
Utawaingiza na kuwapandikiza juu ya mlima wa urithi wako: hapo mahali, Ee Bwana, ulipopafanya kuwa makao yako, mahali patakatifu, Ee Bwana, ulipopajenga kwa mikono yako.
18
Bwana atatawala milele na milele.”
19
Farasi wa Farao, magari yake ya vita na wapanda farasi wake walipoingia baharini, Bwana aliyarudisha maji ya bahari yakawafunika, lakini wana wa Israeli walipita baharini mahali pakavu.
20
Kisha Miriamu yule nabii mke, ndugu yake Aroni, akachukua matari mkononi mwake na wanawake wote wakamfuata na matari yao wakicheza.
21
Miriamu akawaimbia: “Mwimbieni Bwana, kwa maana ametukuka sana. Farasi na mpanda farasi amewatosa baharini.”
22
Kisha Mose akawaongoza Israeli kutoka Bahari ya Shamu na kuingia katika Jangwa la Shuri. Kwa siku tatu walisafiri jangwani bila kupata maji.
23
Walipofika Mara, hawakuweza kunywa maji yake kwa sababu yalikuwa machungu. (Ndiyo sababu mahali hapo panaitwa Mara)
24
Kwa hiyo watu wakamnungʼunikia Mose, wakisema, “Tunywe nini?”
25
Ndipo Mose akamlilia Bwana, naye Bwana akamwonyesha kipande cha mti. Akakitupa ndani ya maji, nayo maji yakawa matamu. Huko Bwana akawapa amri na sheria na huko akawajaribu.
26
Mungu akasema, “Kama mkisikiliza kwa bidii sauti ya Bwana Mungu wenu na kuyafanya yaliyo sawa machoni pake, kama mkiyatii maagizo yake na kuzishika amri zake zote, sitaleta juu yenu ugonjwa wowote niliowaletea Wamisri, kwa kuwa Mimi ndimi Bwana, niwaponyaye.”
27
Kisha wakafika Elimu, mahali palipokuwa na chemchemi kumi na mbili, na miti sabini ya mitende, wakapiga kambi huko karibu na maji.
Maandiko ya Biblia: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu)™, © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. · CC BY-SA 4.0“Biblica” is a trademark registered in the United States Patent and Trademark Office by Biblica, Inc., used with permission.
Settings