Skip to content
Esta 1:13-22

Esta 1:13-22

13
Kwa kuwa ilikuwa desturi ya mfalme kupata ushauri kwa wataalamu katika mambo ya sheria na haki, alizungumza na watu wenye busara, ambao walijua nyakati,
14
nao waliokuwa karibu na mfalme ni Karshena, Shethari, Admatha, Tarshishi, Meresi, Marsena na Memukani, wakuu saba wa Uajemi na Umedi waliokuwa na nafasi ya pekee kwa mfalme nao walikuwa na vyeo vya juu kabisa katika utawala wake.
15
Mfalme akauliza, “Kulingana na sheria, Malkia Vashti anapaswa kutendewa nini? Malkia hakutii amri ya Mfalme Ahasuero ambayo matowashi walimpelekea.”
16
Kisha Memukani akajibu mbele ya mfalme na wakuu, “Malkia Vashti si kwamba amemkosea mfalme tu bali pia amewakosea wakuu wote na watu wa himaya yote ya Mfalme Ahasuero.
17
Kwa maana tendo hili la malkia litajulikana kwa wanawake wote, kwa hiyo watawadharau waume zao na kusema, ‘Mfalme Ahasuero aliagiza Malkia Vashti aletwe mbele yake, lakini alikataa.’
18
Leo hii wanawake wa wakuu wa Uajemi na Umedi ambao wamesikia juu ya tabia ya malkia watawatendea wakuu wote wa mfalme vivyo hivyo. Hapatakuwepo na mwisho wa dharau na magomvi.
19
“Kwa hiyo, kama itampendeza mfalme, atoe amri ya kifalme na iandikwe katika sheria ya Uajemi na Umedi, ambayo haitabadilika, kwamba Vashti kamwe asije tena mbele ya Mfalme Ahasuero. Pia mfalme na atoe hiyo nafasi yake ya umalkia kwa mwanamke mwingine aliye bora kumliko yeye.
20
Kisha mbiu hii ya mfalme itakapotangazwa katika himaya yake iliyo kubwa sana, wanawake wote watawaheshimu waume zao, kuanzia mdogo hadi mkubwa.”
21
Mfalme na wakuu wake walipendezwa na shauri hili, hivyo basi mfalme akafanya kama Memukani alivyopendekeza.
22
Alipeleka barua katika sehemu zote za ufalme wake, kwa kila jimbo kwa maandishi yake mwenyewe na kwa kila watu katika lugha yao wenyewe, akitangaza kwa msemo wa kila watu kwamba inampasa kila mwanaume kuwa mtawala wa nyumba yake mwenyewe.
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Options