2 Nyakati 30:1-9
1
Hezekia akatuma ujumbe kuwaita Israeli wote na Yuda, pia akaandika barua kwa Efraimu na Manase, kuwakaribisha ili waje hekaluni mwa Bwana huko Yerusalemu kuadhimisha Pasaka kwa Bwana, Mungu wa Israeli.
2
Mfalme na maafisa wake pamoja na kusanyiko lote katika Yerusalemu waliamua kuadhimisha Pasaka katika mwezi wa pili.
3
Kwa sababu makuhani hawakuwa wamejitakasa idadi ya kutosha na watu wakawa hawajakusanyika huko Yerusalemu, hawakuwa wameweza kuadhimisha Pasaka kwa wakati wake wa kawaida.
4
Mpango huu ukaonekana wafaa kwa mfalme na kusanyiko lote.
5
Wakaamua kupeleka tangazo Israeli kote, kuanzia Beer-Sheba hadi Dani, wakiwaita watu waje Yerusalemu kuadhimisha Pasaka ya Bwana, Mungu wa Israeli. Ilikuwa haijaadhimishwa na idadi kubwa ya watu kama hiyo kufuatana na yale yaliyokuwa yameandikwa.
6
Kwa amri ya mfalme, matarishi wakapita katika Israeli na Yuda kote wakiwa na barua kutoka kwa mfalme na kutoka kwa maafisa wake zikisema: “Watu wa Israeli, mrudieni Bwana, Mungu wa Abrahamu, Isaki na Israeli, ili naye awarudie ninyi mliosalia, mlionusurika kutoka mikononi mwa wafalme wa Ashuru.
7
Msiwe kama baba zenu na ndugu zenu, ambao hawakuwa waaminifu kwa Bwana, Mungu wa baba zao, hivyo akawafanya kitu cha kushangaza kama mnavyoona.
8
Msiwe na shingo ngumu, kama baba zenu walivyokuwa, bali nyenyekeeni kwa Bwana. Njooni mahali patakatifu, alipopatakasa milele. Mtumikieni Bwana Mungu wenu, ili hasira yake kali igeuziwe mbali nanyi.
9
Kama mkimrudia Bwana ndipo wale ndugu zenu waliotekwa pamoja na watoto wenu watakapoonewa huruma na wale waliowateka na kuwaachia warudi katika nchi hii, kwa kuwa Bwana Mungu wenu ni mwenye neema na huruma, hatageuzia uso wake mbali nanyi kama ninyi mkimrudia yeye.”
Settings