1 Wafalme 6:14-28
14
Basi Solomoni akajenga Hekalu na kulikamilisha.
15
Akazifunika kuta zake za ndani kwa mbao za mierezi, akizipigilia ukutani kuanzia sakafuni mwa Hekalu hadi kwenye dari na kufunika sakafu ya Hekalu kwa mbao za misunobari.
16
Akagawa dhiraa ishirini sehemu ya nyuma ya Hekalu kwa mbao za mierezi kuanzia kwenye sakafu hadi darini ili kufanya sehemu takatifu ya ndani, yaani Patakatifu pa Patakatifu.
17
Ukumbi mkubwa uliokuwa mbele ya chumba hiki ndio ulikuwa na urefu wa dhiraa arobaini.
18
Hekalu ndani ilikuwa ya mierezi iliyonakshiwa mifano ya maboga na maua yaliyochanua. Kila kitu kilikuwa cha mwerezi, hakuna jiwe ambalo lilionekana.
19
Ndani ya Hekalu akatengeneza sehemu takatifu ya ndani, kwa ajili ya kuweka Sanduku la Agano la Bwana.
20
Sehemu takatifu ya ndani ilikuwa na upana, urefu na kimo cha dhiraa ishirini ndani kwa ndani. Akaifunika ndani kwa dhahabu safi, pia akaifunika madhabahu ya mierezi vivyo hivyo.
21
Solomoni akaifunika sehemu ya ndani ya Hekalu kwa dhahabu safi, naye akaitandaza mikufu ya dhahabu kutoka upande moja hadi ule mwingine mbele ya Patakatifu pa Patakatifu, ambako palifunikwa kwa dhahabu.
22
Basi akafunika sehemu yote ya ndani kwa dhahabu. Pia akafunika madhabahu yale yaliyokuwa ndani ya Patakatifu pa Patakatifu kwa dhahabu.
23
Katika Patakatifu pa Patakatifu akatengeneza makerubi wawili kwa mzeituni, kila moja likiwa na dhiraa kumi kwenda juu.
24
Bawa moja la kerubi wa kwanza lilikuwa na urefu wa dhiraa tano na bawa jingine dhiraa tano, hivyo urefu kutoka ncha ya bawa moja hadi ncha ya bawa jingine ulikuwa dhiraa kumi.
25
Kerubi wa pili alikuwa na urefu wa dhiraa kumi pia, hivyo makerubi hao wawili walifanana kwa vipimo na kwa umbo.
26
Kimo cha kila kerubi kilikuwa dhiraa kumi.
27
Aliwaweka makerubi hao ndani ya Patakatifu pa Patakatifu pa Hekalu, mabawa yake yakiwa yamekunjuliwa. Bawa la kerubi mmoja liligusa ukuta mmoja, wakati bawa la yule mwingine liligusa ukuta mwingine, nayo mabawa yao mengine yaligusana katikati ya chumba.
28
Akafunika wale makerubi kwa dhahabu.
Settings