Skip to content
1 Wafalme 6:1-10

1 Wafalme 6:1-10

1
Katika mwaka wa 480 baada ya Waisraeli kutoka nchi ya Misri, katika mwaka wa nne wa utawala wa Solomoni katika Israeli, katika mwezi wa Zivu, ambao ndio mwezi wa pili, alianza kujenga Hekalu la Bwana.
2
Hekalu hilo Mfalme Solomoni alilojenga kwa ajili ya Bwana lilikuwa na urefu wa dhiraa sitini, upana wa dhiraa ishirini na kimo cha dhiraa thelathini kwenda juu.
3
Baraza ya mbele ya Hekalu ilienea dhiraa ishirini kulingana na upana wa Hekalu na kujitokeza dhiraa kumi mbele ya Hekalu.
4
Akatengeneza madirisha membamba yenye vidirisha vidogo vya juu katika Hekalu.
5
Akafanyiza vyumba vya pembeni kulizunguka Hekalu lote vikishikamana na kuta za Hekalu na za Patakatifu pa Patakatifu.
6
Ghorofa ya chini kabisa ilikuwa na upana wa dhiraa tano, ya kati ilikuwa dhiraa sita na ya tatu ilikuwa dhiraa saba. Kuzunguka ukuta wa nje wa Hekalu akapunguza ukuta pande zote ili boriti zisishikane kwenye kuta za Hekalu.
7
Katika kujenga Hekalu, yalitumika tu mawe yaliyochongwa huko machimboni, wala hakuna nyundo, patasi au chombo kingine chochote cha chuma kilichosikika sauti yake katika eneo la ujenzi wa Hekalu wakati lilipokuwa likijengwa.
8
Ingilio la ghorofa ya chini kabisa lilikuwa upande wa kusini wa Hekalu, ngazi ilielekea ghorofa ya kati na kutokea hapo ilielekea hadi ghorofa ya tatu.
9
Basi Solomoni akajenga Hekalu na kulikamilisha, akiliweka paa za boriti na mbao za mierezi.
10
Mfalme Solomoni akajenga vyumba vya pembeni kuzunguka Hekalu lote. Kimo cha kila kimoja kilikuwa dhiraa tano. Navyo vilikuwa vimeunganishwa na Hekalu kwa boriti za mierezi.
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Options