1 Nyakati 21:15-27
15
Mungu akapeleka malaika kuangamiza Yerusalemu. Lakini malaika alipokuwa akifanya hivyo, Bwana akaona na akahuzunika kwa sababu ya maafa, akamwambia yule malaika aliyekuwa anaangamiza watu, “Yatosha! Rudisha mkono wako.” Wakati huo malaika wa Bwana alikuwa amesimama katika sakafu ya kupuria nafaka ya Arauna Myebusi.
16
Daudi akayainua macho yake akamwona huyo malaika wa Bwana akiwa amesimama katikati ya mbingu na dunia, naye ameunyoosha upanga wake juu ya Yerusalemu tayari kuangamiza. Kisha Daudi na wazee, waliokuwa wamevaa nguo za gunia, wakaanguka kifudifudi.
17
Daudi akamwambia Mungu, “Je, si mimi ndiye niliyeamuru watu wahesabiwe? Mimi ndiye niliyetenda dhambi na kukosa. Hawa ni kondoo tu. Wamefanya nini? Ee Bwana, Mungu wangu, mkono wako na uwe juu yangu mimi na jamaa yangu, lakini usiache tauni hii iendelee juu ya watu wako.”
18
Kisha malaika wa Bwana akamwamuru Gadi amwambie Daudi apande na kumjengea Bwana madhabahu kwenye sakafu ya kupuria nafaka ya Arauna Myebusi.
19
Kwa hiyo Daudi akakwea, akalitii lile neno ambalo Gadi alikuwa amelisema katika jina la Bwana.
20
Arauna alipokuwa akipura ngano, akageuka akamwona yule malaika. Wanawe wanne waliokuwa pamoja naye wakajificha, yeye akaendelea kupura ngano.
21
Kisha Daudi akakaribia, Arauna alipotazama na kumwona, akaondoka kwenye uwanja wa kupuria nafaka akamsujudia Daudi akiuinamisha uso wake ardhini.
22
Daudi akamwambia, “Nipatie huu uwanja wako wa kupuria nafaka ili niweze kujenga madhabahu ya Bwana tauni ipate kukomeshwa katika watu. Niuzie kwa bei yake kamili.”
23
Arauna akamwambia Daudi, “Uchukue huo uwanja. Mfalme bwana wangu na afanye lolote analopenda. Tazama, nitatoa maksai kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, vifaa vya kupuria kuwa kuni, pamoja na ngano kwa ajili ya dhabihu ya nafaka. Natoa hivi vyote.”
24
Lakini Mfalme Daudi akamjibu Arauna, “La hasha! Lakini ninasisitiza kwamba nitalipa bei yake kamili. Sitachukua kilicho chako kwa ajili ya Bwana au kutoa sadaka ya kuteketezwa ambayo hainigharimu chochote.”
25
Basi Daudi akamlipa Arauna shekeli za dhahabu 600 kwa ajili ya ule uwanja.
26
Kisha Daudi akamjengea Bwana madhabahu mahali hapo, na kutoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani. Akamwita Bwana naye Bwana akajibu maombi yake kwa moto toka mbinguni juu ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa.
27
Kisha Bwana akanena na yule malaika, naye akarudisha upanga wake katika ala yake.
Settings