1 Nyakati 19:6-15
6
Waamoni walipotambua kuwa wamekuwa machukizo kwa Daudi, Hanuni na Waamoni wakatuma talanta 1,000 za fedha ili kukodisha magari ya vita pamoja na waendeshaji wa hayo magari ya kukokotwa na farasi, kutoka Aramu-Naharaimu, Aramu-Maaka na Soba.
7
Wakakodisha magari ya vita 32,000 yakiwa na waendeshaji wake, pamoja na mfalme wa Maaka na vikosi vyake, wakaja na kupiga kambi karibu na Medeba. Waamoni nao wakakusanyika toka miji yao, wakatoka ili kupigana vita.
8
Daudi aliposikia jambo hili, akamtuma Yoabu na jeshi lote la wapiganaji.
9
Waamoni wakatoka wakajipanga wakiwa tayari kwa vita langoni la mji wao, wakati wale wafalme wengine waliokuja nao walijipanga kwa vita uwanjani.
10
Yoabu akaona kuwa mbele yake na nyuma yake kumepangwa vita; kwa hiyo akachagua baadhi ya vikosi vilivyo bora sana katika Israeli akavipanga dhidi ya Waaramu.
11
Akawaweka wale wanajeshi wengine waliobaki chini ya amri ya Abishai ndugu yake, nao wakapangwa ili wakabiliane na Waamoni.
12
Yoabu akasema, “Kama Waaramu watanizidi nguvu, basi itakupasa wewe unisaidie; lakini kama Waamoni watakuzidi nguvu, basi mimi nitakusaidia.
13
Uwe hodari na tupigane kwa ujasiri kwa ajili ya watu wetu na miji ya Mungu wetu. Bwana atafanya lile lililo jema machoni pake.”
14
Basi Yoabu na vikosi vyake wakasonga mbele kupigana na Waaramu, nao Waaramu wakakimbia mbele yake.
15
Waamoni walipoona Waaramu wanakimbia, nao pia wakakimbia mbele ya nduguye Abishai na kuingia ndani ya mji. Basi Yoabu akarudi Yerusalemu.
Settings