Zaburi 73:1-17
1
Zaburi ya Asafu. Hakika Mungu ni mwema kwa Israeli, kwa wale ambao mioyo yao ni safi.
2
Bali kwangu mimi, miguu yangu ilikuwa karibu kuteleza; nilikuwa karibu mguu wangu kuachia uliposimama.
3
Kwa maana niliwaonea wivu wenye kujivuna nilipoona kufanikiwa kwa waovu.
4
Wao hawana taabu, miili yao ina afya na nguvu.
5
Hawapati shida zinazowataabisha watu wengine, wala hawapati mapigo kama wanadamu wengine.
6
Kwa hiyo kiburi ni mkufu wao, wamejivika jeuri.
7
Uovu hutoka katika mioyo yao iliyokufa ganzi, majivuno maovu kutoka mioyoni mwao hauna kikomo.
8
Hudhihaki na kusema kwa ukorofi, katika majivuno yao wanatishia kutesa.
9
Vinywa vyao huweka madai hata kwa mbingu, nazo ndimi zao humiliki duniani.
10
Kwa hiyo watu wao huwageukia na kunywa maji tele.
11
Wanasema, “Mungu awezaje kujua? Je, Yeye Aliye Juu Sana anayo maarifa?”
12
Hivi ndivyo walivyo waovu: siku zote hawajali, wanaongezeka katika utajiri.
13
Hakika nimeuweka moyo wangu safi bure, ni bure nimenawa mikono yangu nisiwe na hatia.
14
Mchana kutwa nimetaabika, nimeadhibiwa kila asubuhi.
15
Kama ningesema, “Nitasema hivi,” ningelikuwa nimewasaliti watoto wako.
16
Nilipojaribu kuelewa haya yote, yalikuwa magumu kwangu kuelewa.
17
Mpaka nilipoingia patakatifu pa Mungu, ndipo nilipotambua mwisho wao.
Settings