Skip to content
Mithali 30:15-31

Mithali 30:15-31

15
“Mruba anao binti wawili waliao, ‘Nipe! Nipe!’ “Kuna vitu vitatu visivyotosheka kamwe, naam, viko vinne visivyosema, ‘Yatosha!’:
16
Ni kaburi, tumbo lisilozaa, nchi isiyoshiba maji kamwe, na moto, usiosema kamwe, ‘Yatosha!’
17
“Jicho lile limdhihakilo baba, lile linalodharau kumtii mama, litangʼolewa na kunguru wa bondeni, litaliwa na tai.
18
“Kuna vitu vitatu vinavyonishangaza sana, naam, vinne nisivyovielewa:
19
Ni mwendo wa tai katika anga, mwendo wa nyoka juu ya mwamba, mwendo wa meli katika maji makuu ya bahari, nao mwendo wa mtu pamoja na msichana.
20
“Huu ndio mwendo wa mwanamke mzinzi, hula akapangusa kinywa chake na kusema, ‘Sikufanya chochote kibaya.’
21
“Kwa mambo matatu nchi hutetemeka, naam, kwa mambo manne haiwezi kuvumilia:
22
Mtumwa awapo mfalme, mpumbavu ashibapo chakula,
23
mwanamke asiyependwa aolewapo, naye mtumishi wa kike achukuapo nafasi ya bibi yake.
24
“Vitu vinne duniani vilivyo vidogo, lakini vina akili nyingi sana:
25
Mchwa ni viumbe wenye nguvu ndogo, hata hivyo hujiwekea akiba ya chakula chao wakati wa kiangazi.
26
Pelele ni viumbe vyenye uwezo mdogo hata hivyo hujitengenezea nyumba zao kwenye miamba.
27
Nzige hawana mfalme, hata hivyo huenda pamoja vikosi vikosi.
28
Mjusi anaweza kushikwa kwa mkono, hata hivyo huonekana katika majumba ya kifalme.
29
“Viko vitu vitatu ambavyo vinapendeza katika mwendo wao, naam, vinne ambavyo hutembea kwa mwendo wa madaha:
30
simba, mwenye nguvu miongoni mwa wanyama, asiyerudi nyuma kwa chochote;
31
jogoo atembeaye kwa maringo, pia beberu, naye mfalme pamoja na jeshi lake lililomzunguka.
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Options