Obadia 1:1-8
1
Maono ya Obadia. Hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi kuhusu Edomu: Tumesikia ujumbe kutoka kwa Bwana: Mjumbe alitumwa kwa mataifa kusema, “Inukeni, twendeni tukapigane vita dhidi yake.”
2
“Angalieni, nitawafanya wadogo miongoni mwa mataifa, mtadharauliwa kabisa.
3
Kiburi cha moyo wako kimekudanganya, wewe unayeishi katika majabali ya miamba na kufanya makao yako juu, wewe unayejiambia mwenyewe, ‘Ni nani awezaye kunishusha chini?’
4
Ingawa unapaa juu kama tai na kufanya kiota chako kati ya nyota, nitakushusha chini kutoka huko,” asema Bwana.
5
“Ikiwa wevi wangekuja kwako, ikiwa wanyangʼanyi wangekujia usiku: Lo! Tazama ni maafa kiasi gani yangekuwa yanakungojea: je, si wangeiba tu kiasi ambacho wangehitaji? Kama wachuma zabibu wangekuja kwako, je, wasingebakiza zabibu chache?
6
Lakini tazama jinsi Esau atakavyotekwa, jinsi hazina zake zilizofichwa zitatekwa nyara!
7
Wote ulioungana nao watakufukuza hadi mpakani, rafiki zako watakudanganya na kukushinda, wale wanaokula mkate wako watakutegea mtego, lakini hutaweza kuugundua.
8
“Katika siku hiyo,” asema Bwana, “je, sitaangamiza watu wenye hekima wa Edomu, watu wenye ufahamu katika milima ya Esau?
Settings