Waamuzi 9:45-57
45
Siku hiyo nzima Abimeleki akazidisha mashambulizi yake dhidi ya mji hadi akawa ameuteka na kuwaua watu wa huo mji. Kisha akauangamiza mji na kusambaza chumvi juu yake.
46
Kwa kusikia jambo hili watu wote katika mnara wa Shekemu, wakaingia kwenye ngome ya hekalu la El-Berithi.
47
Abimeleki aliposikia kuwa wamekusanyika huko,
48
yeye na watu wake wote wakakwea kwenye Mlima Salmoni. Abimeleki akachukua shoka, akakata baadhi ya matawi, ambayo aliyachukua mabegani. Akawaagiza wale watu waliokuwa pamoja naye kuwa, “Fanyeni kile mlichoona mimi nikifanya!”
49
Basi watu wote wakakata matawi na kumfuata Abimeleki. Wakayakusanya hayo matawi juu ya ngome na kuitia moto ili kuwachoma wale watu wote waliokuwa ndani yake. Hivyo watu wote katika mnara wa Shekemu, karibia watu 1,000 waume kwa wake, pia wakafa.
50
Baadaye Abimeleki akaenda Thebesi na kuuzingira kwa jeshi na kuuteka.
51
Hata hivyo, ndani ya huo mji kulikuwa na mnara imara, ambako watu wote wa mji wanaume na wanawake, watu wote wa mji, walikimbilia ndani yake. Wakajifungia ndani yake na kupanda juu ya paa la mnara.
52
Abimeleki akaja kwenye ule mnara na kuushambulia, lakini alipokaribia kwenye ingilio la mnara ili kuuchoma kwa moto,
53
mwanamke mmoja akaangusha sehemu ya juu ya jiwe la kusagia juu ya kichwa cha Abimeleki, likapasua fuvu la kichwa chake.
54
Akamwita kwa haraka kijana yule aliyechukua silaha zake, na kumwambia, “Chukua upanga wako na uniue, watu wasije wakasema kwamba, ‘Mwanamke amemuua.’ ” Basi yule kijana akamchoma upanga, naye akafa.
55
Waisraeli walipoona kuwa Abimeleki amekufa, kila mtu akaenda nyumbani kwake.
56
Hivyo ndivyo Mungu alivyolipiza uovu ule ambao Abimeleki alikuwa ameutenda kwa baba yake kwa kuwaua ndugu zake sabini.
57
Mungu akawapatiliza watu wa Shekemu uovu wao juu ya vichwa vyao, na juu yao ikaja laana ya Yothamu mwana wa Yerub-Baali.
Settings