Waamuzi 16:1-10
1
Siku moja Samsoni alienda Gaza, akamwona mwanamke kahaba, naye akaingia kwake.
2
Watu wa Gaza wakaambiwa, “Samsoni amekuja huku!” Hivyo wakapazingira mahali pale nao wakamvizia usiku kucha, penye lango la mji. Wakanyamaza kimya usiku kucha, wakisema, “Tumvizie hadi mapambazuko, ndipo tutamuua.”
3
Samsoni akalala mpaka usiku wa manane. Akaondoka katikati ya usiku, akashika milango ya lango la mji pamoja na miimo yake miwili, akaingʼoa, makomeo yake na vyote. Akaviweka mabegani mwake na kuvipeleka mpaka kwenye kilele cha mlima ule unaokabili Hebroni.
4
Baada ya hayo akampenda mwanamke mmoja katika Bonde la Soreki aliyeitwa Delila.
5
Viongozi wa Wafilisti wakamwendea yule mwanamke na kumwambia, “Umbembeleze ili upate kujua siri za nguvu zake zilizo nyingi na jinsi tutakavyoweza kumshinda ili tuweze kumfunga na kumtiisha. Nasi kila mmoja wetu tutakupa shekeli 1,100 za fedha.”
6
Hivyo Delila akamwambia Samsoni, “Naomba niambie siri ya hizi nguvu zako nyingi na jinsi utakavyoweza kufungwa ili kukutiisha.”
7
Samsoni akamjibu, “Kama wakinifunga kwa kamba saba za upinde ambazo hazijakauka bado, hapo ndipo nitakapokuwa dhaifu kama mtu mwingine yeyote.”
8
Viongozi wa Wafilisti wakamletea yule mwanamke kamba saba za upinde ambazo hazijakauka bado, akamfunga nazo Samsoni.
9
Wakati watu wakiwa wanamvizia katika chumba cha ndani, yule mwanamke akamwambia, “Samsoni, Wafilisti wanakujia!” Lakini yeye akazikata zile kamba za upinde, kama vile uzi wa pamba unapoguswa na moto. Hivyo siri ya nguvu zake haikujulikana.
10
Ndipo Delila akamwambia Samsoni, “Umenifanyia mzaha na kuniambia uongo. Tafadhali niambie waweza kufungwa kwa kitu gani?”
Maandiko ya Biblia: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu)™, © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. · CC BY-SA 4.0“Biblica” is a trademark registered in the United States Patent and Trademark Office by Biblica, Inc., used with permission.
Settings