Skip to content
Yoshua 10:13-37

Yoshua 10:13-37

13
Hivyo jua likasimama, nao mwezi ukatulia, hadi taifa hilo lilipokwisha kujilipizia kisasi kwa adui wake, kama ilivyoandikwa katika Kitabu cha Yashari. Jua likasimama kimya katikati ya mbingu, likachelewa kuzama muda wa siku moja nzima.
14
Haijakuwepo siku nyingine kama hiyo kabla au baada, siku ambayo Bwana alimsikiliza mwanadamu. Hakika Bwana alikuwa akiwapigania Israeli.
15
Ndipo Yoshua akarudi kambini huko Gilgali pamoja na Israeli yote.
16
Basi wale wafalme watano wakawa wamekimbia kujificha kwenye pango huko Makeda.
17
Yoshua alipoambiwa kuwa wafalme hao watano wamekutwa wakiwa wamejificha ndani ya pango huko Makeda,
18
akasema, “Vingirisheni mawe makubwa kwenye mdomo wa hilo pango, tena wekeni walinzi wa kulilinda.
19
Lakini msiwaache! Wafuatieni adui zenu, washambulieni kutoka nyuma, wala msiwaache wafike kwenye miji yao, kwa kuwa Bwana Mungu wenu amewatia mkononi mwenu.”
20
Hivyo Yoshua pamoja na Waisraeli wakawaangamiza kabisa karibu wote, lakini wachache waliosalia walifika kwenye miji yao yenye maboma.
21
Basi jeshi lote likarudi salama kwa Yoshua huko kambini Makeda, na hakuna yeyote aliyetoa neno kinyume cha Waisraeli.
22
Ndipo Yoshua akasema, “Haya fungueni mdomo wa pango, mniletee hao wafalme watano.”
23
Kwa hiyo wakawatoa hao wafalme watano nje ya pango: wafalme wa Yerusalemu, Hebroni, Yarmuthi, Lakishi na Egloni.
24
Walipokuwa wamewaleta hawa wafalme kwa Yoshua, akawaita watu wote wa Israeli, na kuwaambia majemadari wa vita waliokwenda pamoja naye, “Njooni hapa mweke nyayo zenu juu ya shingo za hawa wafalme.” Basi wakaja wakaweka nyayo zao shingoni.
25
Yoshua akawaambia, “Msiogope, wala msivunjike moyo. Kuweni hodari na wenye ushujaa. Hili ndilo Bwana atakalowatendea adui zenu wote mnaokwenda kupigana nao.”
26
Ndipo Yoshua akawapiga na kuwaua wale wafalme na kuwatundika juu ya miti mitano, nao wakaachwa wakiningʼinia juu ya ile miti hadi jioni.
27
Wakati wa kuzama jua Yoshua akaamuru, nao wakawashusha kutoka kwenye ile miti na kuwatupa kwenye lile pango ambalo walikuwa wamejificha. Kwenye mdomo wa lile pango wakaweka mawe makubwa, ambayo yapo hadi leo.
28
Siku ile Yoshua akateka Makeda. Akamuua kila mmoja katika ule mji, pamoja na mfalme wake kwa upanga. Hakubakiza mtu yeyote. Akamfanyia mfalme wa Makeda kama vile alivyokuwa amemfanyia mfalme wa Yeriko.
29
Ndipo Yoshua akaondoka Makeda akiwa pamoja na Israeli yote mpaka mji wa Libna na kuushambulia.
30
Bwana pia akautia huo mji wa Libna pamoja na mfalme wake mikononi mwa Israeli. Yoshua akaangamiza ule mji na kila mtu aliyekuwa ndani yake kwa upanga. Hakubakiza huko mtu yeyote. Akamfanyia mfalme wa Libna kama alivyokuwa amemfanyia mfalme wa Yeriko.
31
Kisha Yoshua akaondoka Libna kwenda Lakishi akiwa pamoja na Israeli yote; wakajipanga dhidi yake na kuushambulia.
32
Bwana akautia Lakishi mikononi mwa Israeli, Yoshua akauteka siku ya pili. Yoshua akauangamiza mji na kila kilichokuwa ndani yake kwa upanga, kama tu vile alivyokuwa ameufanyia mji wa Libna.
33
Wakati huo huo, Horamu mfalme wa Gezeri alikuwa amepanda ili kusaidia Lakishi, lakini Yoshua akamshinda pamoja na jeshi lake, hadi hapakubakia mtu yeyote.
34
Ndipo Yoshua akaondoka Lakishi kwenda Egloni akiwa pamoja na Israeli yote; wakajipanga dhidi yake na kuushambulia.
35
Wakauteka mji huo siku ile ile, wakaupiga kwa upanga na kumwangamiza kila mmoja aliyekuwa ndani yake, kama vile walivyokuwa wameufanyia Lakishi.
36
Kisha Yoshua akapanda kutoka Egloni kwenda Hebroni akiwa pamoja na Israeli yote na kuushambulia.
37
Wakauteka mji na kuupiga kwa upanga, pamoja na mfalme wake, vijiji vyake na kila mmoja aliyekuwa ndani yake. Hawakubakiza mtu yeyote. Kama vile huko Egloni, waliuangamiza kabisa pamoja na kila mmoja aliyekuwa ndani yake.

Maandiko ya Biblia: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu)™, © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. · CC BY-SA 4.0“Biblica” is a trademark registered in the United States Patent and Trademark Office by Biblica, Inc., used with permission.

Settings

Reading style

Typeface

Font size 19px

Reading width 75 chars

Options