Yeremia 48:1-20
1
Kuhusu Moabu: Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: “Ole wake Nebo, kwa maana utaharibiwa. Kiriathaimu utaaibishwa na kutekwa; Misgabu itaaibishwa na kuvunjavunjwa.
2
Moabu haitasifiwa tena; huko Heshboni watu watafanya shauri baya la anguko lake: ‘Njooni na tuangamize taifa lile.’ Wewe nawe, ee Madmena, utanyamazishwa; upanga utakufuatia.
3
Sikiliza kilio kutoka Horonaimu, kilio cha maangamizi makuu na uharibifu.
4
Moabu utavunjwa, wadogo wake watapiga kelele.
5
Wanapanda kwenda njia ya kuelekea Luhithi, wakilia kwa uchungu wanapotembea, kwenye njia inayoshuka kwenda Horonaimu, kilio cha uchungu kwa ajili ya uharibifu kinasikika.
6
Kimbieni! Okoeni maisha yenu, kuweni kama kichaka jangwani.
7
Kwa kuwa mmetumainia matendo yenu na mali zenu, ninyi pia mtachukuliwa mateka, naye Kemoshi atakwenda uhamishoni, pamoja na makuhani wake na maafisa wake.
8
Mharabu atakuja dhidi ya kila mji, wala hakuna mji utakaookoka. Bonde litaangamizwa na uwanda utaharibiwa, kwa sababu Bwana amesema.
9
Wekeni chumvi kwa ajili ya Moabu, kwa kuwa ataangamizwa; miji yake itakuwa ukiwa, pasipo kuwa na mtu atakayeishi ndani yake.
10
“Alaaniwe yeye afanyaye kazi ya Bwana kwa hila! Alaaniwe yeye auzuiaye upanga wake usimwage damu!
11
“Moabu amestarehe tangu ujana wake, kama divai iliyoachwa kwenye machujo yake, haikumiminwa kutoka chombo kimoja hadi kingine, hajaenda uhamishoni. Kwa hiyo ana ladha ile ile kama aliyokuwa nayo, nayo harufu yake haijabadilika.
12
Lakini siku zinakuja,” asema Bwana, “nitakapotuma watu wamiminao kutoka kwenye magudulia, nao watamimina; wataacha magudulia yake yakiwa matupu na kuvunja mitungi yake.
13
Kisha Moabu atamwonea aibu mungu wao Kemoshi, kama vile nyumba ya Israeli walivyoona aibu walipotegemea mungu wa Betheli.
14
“Mwawezaje kusema, ‘Sisi ni mashujaa, watu jasiri katika vita’?
15
Moabu ataangamizwa na miji yake itavamiwa, vijana wake waume walio bora sana watachinjwa,” asema Mfalme, ambaye jina lake ni Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote.
16
“Kuanguka kwa Moabu kumekaribia, janga kubwa litamjia kwa haraka.
17
Ombolezeni kwa ajili yake, ninyi nyote mnaomzunguka, ninyi nyote mnaojua sifa zake, semeni, ‘Tazama jinsi ilivyovunjika fimbo ya kifalme yenye nguvu, tazama jinsi ilivyovunjika fimbo iliyotukuka!’
18
“Shuka kutoka fahari yako na uketi katika ardhi iliyokauka, enyi wenyeji wa Binti wa Diboni, kwa maana yeye aangamizaye Moabu atakuja dhidi yako, na kuangamiza miji yako iliyozungushiwa maboma.
19
Simama kando ya barabara na utazame, wewe unayeishi Aroeri. Muulize mwanaume anayekimbia na mwanamke anayetoroka, waulize, ‘Kumetokea nini?’
20
Moabu amefedheheshwa, kwa kuwa amevunjavunjwa. Lieni kwa huzuni na kupiga kelele! Tangazeni kando ya Arnoni kwamba Moabu ameangamizwa.
Settings