Skip to content
Isaya 66:7-24

Isaya 66:7-24

7
“Kabla hajasikia utungu, alizaa; kabla hajapata maumivu, alizaa mtoto mwanaume.
8
Ni nani amepata kusikia jambo kama hili? Ni nani amepata kuona mambo kama haya? Je, nchi yaweza kuzaliwa kwa siku moja, au taifa laweza kutokea mara? Mara Sayuni alipoona utungu, alizaa watoto wake.
9
Je, nilete mwana hadi wakati wa kuzaliwa na nisizalishe?” asema Bwana. “Je, nifunge tumbo la uzazi wakati mimi ndiye nizalishaye?” asema Mungu wako.
10
“Shangilieni pamoja na Yerusalemu na mfurahi kwa ajili yake, ninyi nyote mnaompenda, shangilieni kwa nguvu pamoja naye, ninyi nyote mnaoomboleza juu yake.
11
Kwa kuwa mtanyonya na kutosheka katika faraja ya matiti yake; mtakunywa sana, na kuufurahia wingi wa mafuriko ya ustawi wake.”
12
Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana: “Nitamwongezea amani kama mto, nao utajiri wa mataifa kama kijito kifurikacho; utanyonya na kuchukuliwa mikononi mwake na kubembelezwa magotini pake.
13
Kama mama anavyomfariji mtoto wake, ndivyo nitakavyokufariji wewe, nawe utafarijiwa huko Yerusalemu.”
14
Wakati mtakapoona jambo hili, mioyo yenu itashangilia, nanyi mtastawi kama majani; mkono wa Bwana utajulikana kwa watumishi wake, bali ghadhabu yake kali itaonyeshwa kwa adui zake.
15
Tazama, Bwana anakuja na moto, magari yake ya vita ni kama upepo wa kisulisuli, atateremsha hasira yake kwa ghadhabu kali, na karipio lake pamoja na miali ya moto.
16
Kwa maana kwa moto na kwa upanga wake Bwana atatekeleza hukumu juu ya watu wote, nao wengi watakuwa ni wale waliouawa na Bwana.
17
“Watu wote wanaojiweka wakfu na kujitakasa wenyewe ili kwenda bustanini, wakimfuata aliye katikati ya wale ambao hula nyama za nguruwe na panya pamoja na vitu vingine vilivyo machukizo, watafikia mwisho wao pamoja,” asema Bwana.
18
“Nami, kwa sababu ya matendo yao na mawazo yao, niko karibu kuja na kukusanya mataifa yote na lugha zote, nao watakuja na kuuona utukufu wangu.
19
“Nitaweka ishara katikati yao, nami nitapeleka baadhi ya hao walionusurika kwa mataifa, hadi Tarshishi, kwa Puli na Waludi (wanaojulikana kama wapiga upinde), kwa Tubali na Uyunani, hadi visiwa vya mbali ambavyo havijasikia juu ya sifa zangu au kuuona utukufu wangu. Watatangaza utukufu wangu miongoni mwa mataifa.
20
Nao watawaleta ndugu zenu wote, kutoka mataifa yote, mpaka kwenye mlima wangu mtakatifu katika Yerusalemu kama sadaka kwa Bwana, juu ya farasi, katika magari ya vita na magari makubwa, juu ya nyumbu na ngamia,” asema Bwana. “Watawaleta, kama Waisraeli waletavyo sadaka zao za nafaka, katika Hekalu la Bwana, katika vyombo safi kwa kufuata desturi za ibada.
21
Nami nitachagua baadhi yao pia wawe makuhani na Walawi,” asema Bwana.
22
“Kama vile mbingu mpya na nchi mpya ninazozifanya zitakavyodumu mbele zangu,” asema Bwana, “ndivyo jina lenu na wazao wenu watakavyodumu.
23
Kutoka Mwezi Mpya hata mwingine, na kutoka Sabato hadi nyingine, wanadamu wote watakuja na kusujudu mbele zangu,” asema Bwana.
24
“Nao watatoka nje na kuona maiti za wale walioniasi mimi. Funza wao hawatakufa, wala moto wao hautazimika, nao watakuwa kitu cha kuchukiza sana kwa wanadamu wote.”
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Options