Isaya 40:1-11
1
Wafarijini, wafarijini watu wangu, asema Mungu wenu.
2
Sema na Yerusalemu kwa upole, umtangazie kwamba kazi yake ngumu imekamilika, kwamba dhambi yake imefanyiwa fidia, kwamba amepokea kutoka mkononi mwa Bwana maradufu kwa ajili ya dhambi zake zote.
3
Sauti ya mtu aliaye: “Itengenezeni jangwani njia ya Bwana, nyoosheni njia kuu nyikani kwa ajili ya Mungu wetu.
4
Kila bonde litainuliwa, kila mlima na kilima kitashushwa; penye mabonde patanyooshwa, napo palipoparuza patasawazishwa.
5
Utukufu wa Bwana utafunuliwa, nao wanadamu wote watauona pamoja. Kwa maana kinywa cha Bwana kimenena.”
6
Sauti husema, “Piga kelele.” Nami nikasema, “Nipige kelele gani?” “Wanadamu wote ni kama majani, nao utukufu wao wote ni kama maua ya kondeni.
7
Majani hunyauka na maua huanguka, kwa sababu pumzi ya Bwana huyapuliza. Hakika wanadamu ni majani.
8
Majani hunyauka na maua huanguka, lakini neno la Mungu wetu ladumu milele.”
9
Wewe uletaye habari njema Sayuni, panda juu ya mlima mrefu. Wewe uletaye habari njema Yerusalemu, inua sauti yako kwa kupiga kelele, inua sauti, usiogope; iambie miji ya Yuda, “Yuko hapa Mungu wenu!”
10
Tazameni, Bwana Mwenyezi anakuja na nguvu, nao mkono wake ndio utawalao kwa ajili yake. Tazameni, ujira wake u pamoja naye, nayo malipo yake yanafuatana naye.
11
Huchunga kundi lake kama mchungaji wa mifugo: Hukusanya wana-kondoo katika mikono yake na kuwachukua karibu na moyo wake, huwaongoza taratibu wale wanyonyeshao.
Settings