Mwanzo 31:25-35
25
Yakobo alikuwa amepiga hema lake katika nchi ya vilima katika Gileadi wakati Labani alipomkuta, Labani na jamaa yake wakapiga kambi huko pia.
26
Ndipo Labani akamwambia Yakobo, “Umefanya nini? Umenidanganya na umewachukua binti zangu kama mateka katika vita.
27
Kwa nini ulikimbia kwa siri na kunidanganya? Kwa nini hukuniambia ili nikuage kwa furaha na nyimbo za matari na vinubi?
28
Hata hukuniruhusu niwabusu wajukuu zangu na kuwaaga binti zangu. Umefanya kitu cha kipumbavu.
29
Nina uwezo wa kukudhuru, lakini usiku uliopita Mungu wa baba yako alisema nami, akaniambia, ‘Jihadhari, usiseme neno lolote kwa Yakobo liwe zuri au baya.’
30
Sasa umeondoka kwa sababu umetamani kurudi nyumbani kwa baba yako. Lakini kwa nini umeiba miungu yangu?”
31
Yakobo akamjibu Labani, “Niliogopa, kwa sababu nilifikiri ungeweza kuninyangʼanya binti zako kwa nguvu.
32
Lakini kama ukimkuta yeyote aliye na miungu yako, hataishi. Mbele ya jamaa yetu, angalia mwenyewe uone kama kuna chochote chako hapa nilicho nacho, kama kipo, kichukue.” Basi Yakobo hakujua kwamba Raheli alikuwa ameiba hiyo miungu.
33
Kwa hiyo Labani akaingia ndani ya hema la Yakobo na ndani ya hema la Lea na ndani ya hema la watumishi wawili wa kike, lakini hakukuta chochote. Baadaye alipotoka katika hema la Lea, akaingia hema la Raheli.
34
Basi Raheli ndiye alikuwa amechukua ile miungu ya nyumbani kwao na kuiweka katika matandiko ya ngamia na kukalia. Labani akatafuta kila mahali kwenye hema lakini hakupata chochote.
35
Raheli akamwambia baba yake, “Usikasirike, bwana wangu kwa kuwa siwezi kusimama ukiwepo, niko katika hedhi.” Labani akatafuta lakini hakuweza kuipata miungu ya nyumbani kwake.
Settings