Danieli 9:4-19
4
Nikamwomba Bwana Mungu wangu na kutubu: “Ee Bwana, Mungu mkuu na unayetisha, anayeshika agano lake la upendo kwao wanaompenda na kutii maagizo yake,
5
tumetenda dhambi na kufanya mabaya. Tumekuwa waovu na tumeasi; tumegeuka mbali na maagizo yako na sheria zako.
6
Hatukuwasikiliza watumishi wako manabii, ambao kwa jina lako walisema na wafalme wetu, wakuu wetu, baba zetu, na watu wote wa nchi.
7
“Bwana, wewe ni mwenye haki, lakini siku hii ya leo tumefunikwa na aibu: tukiwa wanaume wa Yuda, na watu wa Yerusalemu, na Israeli yote, wote walio karibu na walio mbali, katika nchi zote ulikotutawanya kwa sababu ya kukosa uaminifu kwako.
8
Ee Bwana, sisi na wafalme wetu, wakuu wetu na baba zetu tumefunikwa na aibu kwa sababu tumefanya dhambi dhidi yako.
9
Bwana Mungu wetu ni mwenye rehema na anayesamehe, hata ingawa tumefanya uasi dhidi yake.
10
Hatukumtii Bwana Mungu wetu wala kuzishika sheria alizotupa kupitia kwa watumishi wake manabii.
11
Israeli yote imekosea sheria yako na kugeuka mbali, nao wamekataa kukutii. “Kwa hiyo laana na viapo vya hukumu vilivyoandikwa katika Sheria ya Mose, mtumishi wa Mungu, vimemiminwa juu yetu, kwa sababu tumefanya dhambi dhidi yako.
12
Umetimiza maneno uliyosema dhidi yetu na dhidi ya watawala wetu, kwa kuleta maafa makubwa juu yetu. Chini ya mbingu yote kamwe hapajatendeka kitu kama kile kilichotendeka kwa Yerusalemu.
13
Kama vile ilivyoandikwa katika sheria ya Mose, misiba hii yote imekuja juu yetu, lakini hatujaomba fadhili kwa Bwana Mungu wetu kwa kugeuka kutoka dhambi zetu na kuwa wasikivu katika kweli yake.
14
Bwana hakusita kuleta maafa juu yetu, kwa maana Bwana Mungu wetu ni mwenye haki katika kila afanyalo; lakini hata hivyo hatujamtii.
15
“Sasa, Ee Bwana Mungu wetu, ambaye uliwatoa watu wako Misri kwa mkono wenye nguvu, na ambaye umejifanyia Jina linalodumu mpaka leo, tumetenda dhambi, tumefanya mabaya.
16
Ee Bwana, wewe kwa kadiri ya matendo yako ya haki, ondoa hasira yako na ghadhabu yako juu ya Yerusalemu, mji wako, mlima wako mtakatifu. Dhambi zetu na maovu ya baba zetu yameifanya Yerusalemu na watu wako kitu cha kudharauliwa kwa wale wote wanaotuzunguka.
17
“Basi Mungu wetu, sasa sikia maombi na dua ya mtumishi wako. Ee Bwana, kwa ajili yako angalia kwa huruma ukiwa wa mahali pako patakatifu.
18
Ee Mungu, tega sikio na ukasikie; fumbua macho yako ukaone ukiwa wa mji ule wenye Jina lako. Hatukutolei maombi yetu kwa sababu sisi tuna haki, bali kwa sababu ya rehema zako nyingi.
19
Ee Bwana, sikiliza! Ee Bwana, samehe! Ee Bwana, sikia na ukatende! Kwa ajili yako, Ee Mungu wangu, usikawie, kwa sababu mji wako na watu wako wanaitwa kwa Jina lako.”
Settings