Danieli 4:24-33
24
“Ee mfalme, hii ndiyo tafsiri, na hii ni amri ya Aliye Juu Sana aliyoitoa dhidi ya bwana wangu mfalme:
25
Wewe utafukuzwa mbali na wanadamu, nawe utaishi pamoja na wanyama pori; utakula manyasi kama ngʼombe, na kuloana kwa umande wa mbinguni. Nyakati saba zitapita juu yako, mpaka utakapokubali kuwa Yeye Aliye Juu Sana ndiye anayetawala juu ya falme za wanadamu, naye humtawaza yeyote amtakaye.
26
Amri ya kuacha kisiki pamoja na mizizi yake inamaanisha kwamba ufalme wako utarejezwa kwako utakapokubali kwamba Mbingu ndizo zitawalazo.
27
Kwa hiyo, ee mfalme, uwe radhi kupokea shauri langu: Acha dhambi zako kwa kutenda yaliyo haki, ukaache uovu wako, na uwe na huruma kwa walioonewa. Hivyo itawezekana baada ya hayo, mafanikio yako yakaendelea.”
28
Haya yote yalimpata Mfalme Nebukadneza.
29
Miezi kumi na miwili baadaye, mfalme alipokuwa akitembea juu ya paa la jumba la kifalme la Babeli,
30
alisema, “Je, huu si Babeli mji mkuu nilioujenga kama makao ya kifalme, kwa uwezo wangu mkubwa, na kwa ajili ya utukufu wa enzi yangu?”
31
Maneno hayo yalikuwa bado katika midomo yake wakati sauti ilipokuja kutoka mbinguni, ikisema, “Mfalme Nebukadneza, hiki ndicho kilichoamriwa kwa ajili yako: Mamlaka yako ya ufalme yameondolewa kutoka kwako.
32
Utafukuzwa mbali na wanadamu, ukaishi pamoja na wanyama pori, na utakula manyasi kama ngʼombe. Nyakati saba zitapita juu yako, mpaka utakapokubali kuwa Yeye Aliye Juu Sana ndiye anayetawala juu ya falme za wanadamu, naye humtawaza yeyote amtakaye.”
33
Papo hapo yale yaliyokuwa yamesemwa kuhusu Nebukadneza yakatimia. Alifukuzwa mbali na wanadamu, akala majani kama ngʼombe. Mwili wake uliloweshwa kwa umande wa mbinguni mpaka nywele zake zikakua kama manyoya ya tai na kucha zake kama makucha ya ndege.
Maandiko ya Biblia: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu)™, © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. · CC BY-SA 4.0“Biblica” is a trademark registered in the United States Patent and Trademark Office by Biblica, Inc., used with permission.
Settings